09
Sep
Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo yatua nchini kwa mazungumzo ya uhifadhi
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za MisituTanzania (TFS) itakuwa mwenyeji wa Waziri wa Utalii na Mazingira wa Jamhuri ya Kongo na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo (CBCC), Mhe. Arlette Soudan – Nonault kuanzia tarehe 9 hadi 12 Septemba 2024.
Ziara hii inatoa fursa muhimu ya kukuza ushirikiano na kuongeza uelewa kuhusu changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa rasilimali za maliasili katika bonde la Kongo.
Akizungumza leo Septemba 9, 2024 jijini Dodoma, Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo amesema Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo, iliyoanzishwa Novemba, 2016 wakati wa mkutano wa COP 22 uliofanyika Morocco, ikijumuisha nchi 17, ikiwemo Tanzania.
Anaongeza kuwa lengo kuu la Kamisheni hiyo ni kuimarisha uwezo wa nchi wanachama katika kulinda na kuhifadhi misitu na mito ya Kongo, ambayo ina umuhimu mkubwa katika kudhibiti hali ya hewa duniani na kukuza maendeleo endelevu ya jamii.
Prof. Silayo anasema katika ziara hiyo Waziri na Katibu Mtendaji wa CBCC ameongozana na wajumbe nane ambapo watafanya mkutano na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Pindi Chana pamoja na mazungumzo na mawaziri wa sekta nyingine kama vile Mazingira, Mambo ya Nje, Fedha, Uchumi, na Mipango.
Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Bi. Florantine Mapeine Onotiang, Mkurugenzi Mkuu wa Bonde la Kongo; Bi. Yao Yao Née Aissatou Cisse, Mshauri wa Kimataifa; Bw. Pascual Nguema Nkongo Andeme, Kiongozi wa Kazi katika Ofisi ya Rais wa Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC); Bw. Guy Lié Djombe, Kiongozi wa BDEAC; Bw. Osty Destin Nzonza, Mpigapicha; Bi. Lee Danielle Abiome; na Bw. Kessali Lekouledzela, Msaidizi wa Waziri.
“Ziara hii ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania, ambayo kama mwanachama wa CBCC, inafaidika na utaratibu wa pamoja wa usimamizi wa rasilimali za maliasili, rasilimali fedha, na kuimarisha mifumo ikolojia ya eneo letu.
“Ujumbe huu utasaidia kuimarisha sauti ya Tanzania katika majadiliano ya kimataifa kuhusu usimamizi wa maliasili na mabadiliko ya tabianchi, huku ikichangia uzoefu wake na kupokea maarifa mapya kutoka kwa nchi nyingine wanachama,” anasema.
Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo inajumuisha nchi 17, ambazo ni Angola, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kati ya Afrika, Chad, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea Ikweta, Ufalme wa Morocco, Gabon, Kenya, Rwanda, Sao Tome na Principe, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, na Zambia.