07
Jun
Mzinga wa Nyuki Wavutia Wahadzabe Kili-Fair 2025, TFS Yatangaza Utalii wa Nyuki
Mzinga wa kisasa wa nyuki uliowekwa mezani katika banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) leo umegeuka kivutio kikubwa kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kili-Fair 2025, na kuwashangaza baadhi ya wageni wa kipekee kutoka jamii ya Hadzabe.
Katika tukio hilo, Maafisa Utalii wa TFS, Salome Kivuyo na Yusuph Tango, walitoa maelezo ya kina kuhusu mpango wa “utalii wa nyuki” (apiculture tourism) – mradi mpya unaolenga kuwavutia watalii wa ndani na wa kimataifa kutembelea mizinga, kujifunza kuhusu maisha ya nyuki, na kununua bidhaa halisi za asali ya misitu.
“Tunataka dunia ielewe kuwa Tanzania haiishi tu kwa simba na tembo. Hata wadudu kama nyuki ni sehemu ya urithi wa bioanuai tunaopaswa kuutangaza,” alisema Tango, huku akionyesha mzinga wenye glasi inayoonesha moja kwa moja shughuli za nyuki kwa kijana wa jamii ya Hadzabe aliyeshangazwa na teknolojia hiyo ya kisasa.
Jamii ya Hadzabe ni miongoni mwa wachache duniani wanaoendelea kuishi kwa uwindaji na ukusanyaji wa matunda. Wamejulikana kwa ushirikiano wa kipekee na ndege mdogo aina ya honeyguide, anayewaongoza hadi kwenye mizinga ya nyuki porini. Baada ya kuvuna asali, huacha mabaki ya sega kwa ndege huyo kama “shukrani”.
“Hawa nyuki ni marafiki wetu tangu enzi za mababu. Tunaipongeza TFS kwa kutambua umuhimu wao na kuleta njia mpya za kuendeleza urithi wetu,” alisema kijana huyo kwa kiswahili kibovu.
Maonesho ya Karibu Kili-Fair, ambayo ndiyo makubwa zaidi ya utalii Afrika Mashariki, yamefunguliwa leo katika viwanja vya Magereza Kisongo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko. Akizindua maonesho hayo yenye washiriki zaidi ya 450 kutoka zaidi ya mataifa 30, Dkt. Biteko alisema:
“Kili-Fair 2025 si tu jukwaa la kutangaza vivutio vyetu, bali pia daraja la kuwaunganisha watoa huduma wa ndani na masoko ya kimataifa. Ni nafasi ya kuchochea ajira, mapato na thamani ya rasilimali zetu za kiutamaduni na kiasili.”