16
Jun

JESHI LA UHIFADHI LATAMBA KONGAMANO LA UNUNUZI WA UMMA ARUSHA

Jeshi la Uhifadhi chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) limetumia vyema fursa ya kongamano la tisa la ununuzi wa umma linaloendelea jijini Arusha kwa kuonyesha namna linavyochangia maendeleo ya taifa kupitia usimamizi wa rasilimali za misitu, nyuki na wanyamapori.

Kongamano hilo, linaloandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), linafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kuanzia Juni 14 hadi 17, 2025, likiwa na lengo la kujadili mageuzi ya teknolojia katika sekta ya manunuzi na namna mfumo wa NeST unavyorahisisha upatikanaji wa zabuni kwa makundi maalum.

Akizungumza na Mwananchi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhifadhi na Meneja wa Ununuzi TFS, Fridolin Matembo, amesema mfumo huo umeleta mapinduzi makubwa hasa kwa makundi maalum ambayo awali yalikuwa na changamoto ya kuingia katika mnyororo wa manunuzi.

"Kupitia sheria mpya ya manunuzi Na. 10 ya mwaka 2023 na mfumo wa NeST, tumeweza kuingiza vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kandarasi rasmi badala ya kuwa vibarua wa muda mfupi kama ilivyokuwa awali," alisema Matembo.

Ameeleza kuwa Jeshi la Uhifadhi limegawanyika katika vikosi vinne vya uhifadhi wa Ngorongoro (NCAA), TANAPA, TAWA na kikosi cha TFS ambacho kinasimamia misitu na nyuki, kikiongozwa na Kamishna Prof. Dos Santos Silayo. Kwa mujibu wa Matembo, TFS imeshatoa kazi kwa vikundi maalum vinavyohusika na kuzuia moto, ufugaji nyuki, uvunaji wa miti na maandalizi ya bustani.

"Tunapoweka mikakati ya kuwafikia vikundi hivi moja kwa moja kupitia mfumo wa NeST, tunawajengea uwezo, tunashirikiana na idara ya maendeleo ya jamii ili wasajiliwe rasmi na hatimaye kuingia kwenye zabuni za TFS kwa uwazi na ushindani wa haki," alisisitiza.

Aidha, Matembo amewataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo kila wanapoona shughuli za TFS zikiendelea katika maeneo yao, akisisitiza kuwa taasisi hiyo imejipanga kutoa elimu na kushirikisha wadau wote kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria.

"Kamishna wetu ni mfuatiliaji makini. Tumekuwa tukitekeleza mabadiliko haya kwa vitendo, na kwa sasa vikundi vinafikia maeneo yote nchini ambapo TFS ipo. Mfumo wa NeST unatusaidia kufikia uwazi, ufanisi na uwajibikaji," alieleza.

Kuhusu mafanikio ya kongamano hilo, Matembo amesema mada zilizowasilishwa zimewasaidia watumishi wa umma kuongeza uelewa wao kuhusu mabadiliko ya sheria, moduli mpya kama ya tender board, na namna ya kushughulikia malalamiko ya wazabuni kupitia mifumo ya kidigitali.

"Kwa mfano, masuala ambayo zamani yangepelekwa kwa mikono sasa yanafanyika mtandaoni, jambo ambalo linaongeza uwazi na kupunguza urasimu. TFS, ikiwa na matawi kila wilaya, ni mnufaika mkubwa wa mfumo huu mpya wa manunuzi ya umma," alisema.

Kongamano hilo linatarajiwa kufungwa rasmi Juni 17, huku TFS ikionekana kuwa mfano bora wa taasisi ya umma inayotekeleza mageuzi ya ununuzi kwa vitendo.