21
Mar
RC BABU AONGOZA UPANDAJI WA MITI MOSHI, MICHE 2,000 YAPANDWA NJORO
Moshi
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe Nurdin Babu, ameongoza zoezi la upandaji miti lililohusisha upandaji wa miche 2,000 katika eneo la Njoro, Manispaa ya Moshi, sambamba na utoaji wa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi.
Zoezi hilo lililofanyika Machi 21, 2026, limeandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo Bodi ya Maji Bonde la Mto Pangani, WWF, MIXX by YAS, waandishi wa habari na wadau wengine wa mazingira kupitia Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Mbali na upandaji miti, washiriki pia walizindua documentary maalum inayolenga kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika juhudi za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava, alisisitiza umuhimu wa kutunza miti akieleza kuwa ni nguzo muhimu katika kulinda vyanzo vya maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Utunzaji wa miti si hiari bali ni wajibu wa kila mwananchi, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za ukame na mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema Mzava.
Zoezi hilo lilihusisha pia wahifadhi wa TFS ambao walitia mkazo zaidi katika utoaji wa elimu kwa vitendo kwa wananchi wa Njoro kuhusu umuhimu wa kupanda na kutunza miti.
Kupitia kampeni ya “One Step, One Tree,” wananchi wamehamasishwa kuona kila hatua wanayopiga kama fursa ya kuchangia uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Tofauti na matukio mengi ya aina hiyo, washiriki walieleza kuwa zoezi hilo limejikita zaidi katika ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi na utoaji wa elimu kwa vitendo, hatua inayotajwa kuongeza uelewa na kujenga utamaduni endelevu wa utunzaji wa mazingira.