27
Jul

TFS Yaimarisha Mapambano Dhidi ya Uhalifu wa Misitu kwa Vikosi Maalumu

Na Mwandishi Wetu, Mlele

Mlele, Katavi. Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Alhaj Majid Mwanga amesema mafunzo maalumu ya ukamataji salama na udhibiti wa vikosi vya Rapid Response Team (RRT) yaliyotolewa kwa askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), yamefungua ukurasa mpya katika mapambano dhidi ya wahalifu wa misitu, akisisitiza kuwa enzi za kuidharau TFS zimekwisha.

Akizungumza jana Julai 22, 2026 wakati akifunga mafunzo ya siku 14 yaliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Jeshi la Uhifadhi Mlele, Mhe. Mwanga alisema wahalifu waliokuwa wameizoea "TFS ya kirungu" sasa wanapaswa kutambua kuwa wamekabiliana na askari waliopatiwa mbinu za kisasa za ukamataji salama, udhibiti wa ghasia na mapambano ya karibu bila kutumia nguvu kupita kiasi.

"Wahalifu waliokuwa wameizoea TFS wa kirungu, sasa ni TFS wa karate, TFS yenye mbinu za kudhibiti, TFS waliotimilika na kutahiniwa. Serikali iko pamoja nanyi. Kachapeni kazi bila kumonea mtu, bila kuvunja sheria za nchi, lakini hakikisheni misitu yetu inalindwa," alisema Mhe. Mwanga.

Mkuu huyo wa wilaya alisema Serikali itaendelea kushirikiana na TFS pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha urithi wa taifa unalindwa dhidi ya uvamizi wa wafugaji, wakulima na wavunaji haramu wa mazao ya misitu, huku akitoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na uhalifu huo.

Mwanga pia aliipongeza TFS chini ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, akisema taasisi hiyo imepata mageuzi makubwa yanayoonekana kwa kuongeza idadi ya watumishi, kuboresha maslahi yao na kuongeza vitendea kazi, hatua ambazo zimeimarisha uwezo wa askari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, alieleza kuwa Wilaya ya Mlele imeimarisha udhibiti wa shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu kwa kuweka masharti mapya yanayomtaka kila anayeingia kuvuna mazao ya misitu kuwa na kitambulisho cha NIDA, kibali cha kijiji husika na nyaraka zote za kisheria kabla ya kuruhusiwa kuingia katika hifadhi. Alisema hatua hizo zimelenga kudhibiti wahalifu na wageni wasiokuwa na sifa wanaojihusisha na uharibifu wa misitu.

Awali, Kaimu Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi, PCO Ali Maggid, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa TFS wa kujenga vikosi maalumu vya RRT katika kanda zote saba za wakala ili kuendana na mabadiliko ya mbinu zinazotumiwa na wahalifu wa misitu. Alisisitiza kuwa mafunzo hayo yanazingatia sheria, haki za binadamu na matumizi ya nguvu stahiki katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, Kaimu Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi, PCO Ali Maggid, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuimarisha uwezo wa vikosi maalumu vya Rapid Response Team (RRT) vinavyoundwa katika kanda zote saba za TFS ili kukabiliana na mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu wa misitu.

Alisema wahifadhi hao wamepatiwa mbinu za kisasa za ukamataji salama, udhibiti wa ghasia na matumizi sahihi ya nguvu, huku wakisisitizwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na haki za binadamu.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yameanza kwa askari 40 kutoka Kanda ya Kusini na Kanda ya Magharibi, lakini yataendelea kutolewa kwa vikosi maalumu vya RRT vilivyopo katika kanda zote saba za TFS, kwa kuwa wahalifu wa misitu wamekuwa wakibadilisha mbinu zao na hivyo kulazimu taasisi hiyo kuongeza uwezo wa askari wake kukabiliana na hali hiyo.

PCO. Maggid alisema hifadhi za misitu zinaendelea kukabiliwa na changamoto za uvamizi kwa ajili ya ufugaji, kilimo, makazi na shughuli nyingine haramu, huku baadhi ya watumishi wa TFS wakijeruhiwa na wengine kupoteza maisha wanapotekeleza majukumu yao. Alisema hali hiyo inalazimu askari wa uhifadhi kuendelea kujengewa uwezo ili kukabiliana na wahalifu wanaobadilisha mbinu za uhalifu kila wakati.

Aidha, alisema TFS itaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha rasilimali za misitu na nyuki zinalindwa kwa ufanisi.

Naye Mkufunzi Kiongozi kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, Mrakibu wa Polisi (SP) Fadhili Noel Tambale, alisema mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na TFS yamelenga kuimarisha uwezo wa askari katika ukamataji salama na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo katika kulinda rasilimali za taifa.

Kwa upande wake, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, CR II Jacklyn Gibson Tawale kutoka TFS Kanda ya Magharibi, alisema elimu waliyoipata itawawezesha kukabiliana kwa ufanisi zaidi na uvamizi wa misitu na kutumia mbinu za kisasa kulinda rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.