19
Mar
MITI 3,000 YAPANDWA KULINDA CHANZO CHA MAJI KITETO
Na Mwandishi Wetu, Kiteto
KATIKA kuelekea maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti, wakazi wa Wilaya ya Kiteto wameungana na wataalamu wa misitu kupanda miche 3,000 katika chanzo cha maji kilichopo mji wa Kibaya, ikiwa ni jitihada za kulinda vyanzo vya maji na kurejesha uoto wa asili.
Zoezi hilo limefanyika leo Machi 19, 2026 kwa ushirikiano kati ya TFS Kiteto, Idara ya Maliasili, Idara ya Maji pamoja na wananchi wa eneo hilo. Aidha, sambamba na upandaji huo, miche ya miti na matunda imegawiwa kwa wananchi ili kuhamasisha upandaji endelevu katika kaya zao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, mgeni rasmi aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mheshimiwa Diwani Mohamed Kinyonga, aliwataka wananchi kuhakikisha wanatunza miti iliyopandwa ili kulinda chanzo hicho cha maji kilichoanza kupoteza uhai kutokana na uharibifu wa mazingira.
Alisema uharibifu wa uoto wa asili umekuwa ukichangia kukauka kwa vyanzo vya maji, hivyo hatua ya kupanda miti ni muhimu katika kurejesha hali hiyo na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa jamii.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni: “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuhifadhi kwa Maendeleo ya Taifa.”