22
Mar

MAKAMU WA RAIS AKAGUA BWAWA LA MINDU,ASISITIZA UHIFADHI WA VYANZO VYA MAJI

Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametembelea na kukagua Bwawa la Mindu mkoani Morogoro, ambalo ni chanzo kikuu cha maji safi kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro, na kusisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma hiyo.

Ziara hiyo imefanyika leo, Machi 22, 2026, ikiwa ni sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa yanayofanyika mkoani Morogoro, ambapo Makamu wa Rais ni mgeni rasmi.

Akiwa katika bwawa hilo, Mheshimiwa Nchimbi alijionea hali ya miundombinu na kuelezwa kuhusu mipango ya upanuzi wa bwawa hilo inayolenga kuongeza uwezo wa uzalishaji maji, ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais alipanda mti kuashiria dhamira ya Serikali katika kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji, sambamba na uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa utabiri wa kiasi cha maji katika mito, unaotarajiwa kusaidia kutoa taarifa za mwenendo wa maji kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi miezi mitatu.

Akihutubia viongozi na wananchi katika Viwanja vya Tumbaku, Mheshimiwa Nchimbi alizitaka taasisi zote za umma na binafsi kuchukua hatua madhubuti kulinda mazingira, hususan vyanzo vya maji, na kuhakikisha mifumo ya maji taka haiathiri ubora wa maji safi.

“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa. Ushirikiano wa wadau wote, ikiwemo sekta binafsi, ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji nchini,” alisema.

Katika maadhimisho hayo, Kamishna wa Uhifadhi aliwakilishwa na Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Morogoro, SCO Stanley Kweka, huku Kamanda wa Kanda ya Mashariki akiwakilishwa na SCO Azizi Mhina.