26
Mar

UKEREWE YAFAIDIKA NA UBIA WA TFS, HEKTA 1,050 ZAGEUKA FURSA

Na Mwandishi Wetu, Ukerewe
Machi 25, 2026

Ukerewe imeanza kunufaika na fursa mpya za ajira na ukuaji wa uchumi kufuatia kuimarishwa kwa ubia wa usimamizi wa Shamba la Miti la Ubia la Rubya lenye ukubwa wa hekta 1,050, baada ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kushiriki kikao muhimu cha kupanga mikakati ya pamoja ya uhifadhi na uzalishaji endelevu.

Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe kimeelezwa kuwa hatua ya kimkakati inayolenga kugeuza rasilimali misitu kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi huku ikilinda mazingira na vyanzo vya maji vinavyozunguka ukanda wa Ziwa Victoria.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mhe Christopher Ngubiagai, alipongeza juhudi za TFS akisema zimekuwa na mchango mkubwa katika kulinda mazingira na kuimarisha ustawi wa jamii. Alisisitiza kuwa ubia huo utaongeza tija katika matumizi ya rasilimali na kutoa fursa kwa vijana kujiajiri.

“Ubia huu unaenda kuwa suluhisho la changamoto mbili kwa wakati mmoja, uhifadhi wa mazingira na ajira kwa vijana. Hii ni fursa adhimu kwa Ukerewe,” alisema Mhe Ngubiagai.

Kwa mujibu wa maazimio ya kikao hicho, TFS imekabidhiwa uenyekiti wa ubia huo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za shamba hilo. Nafasi hiyo itashikiliwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali TFS, Dkt. Zainabu Shaban Bungwa.

Kwa upande wa Halmashauri, Kaimu Mwenyekiti atakuwa Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Ndugu Goodluck Mtigandi, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED), huku wadau wengine wakijumuisha wataalamu wa sekta ya misitu na usimamizi wa rasilimali.

Washiriki wengine wa kikao hicho ni pamoja na Mhifadhi wa Shamba la Miti la Rubya, Festo Chaula, Kamanda wa Kanda ya Ziwa kutoka TFS, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ebrantino Mgiye, pamoja na Meneja wa Mashamba kutoka TFS Makao Makuu, Noel Maeda.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya misitu, kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuchochea mapato ya Halmashauri, huku ukitoa ajira kwa mamia ya vijana wa eneo hilo.

Hatua hiyo pia inaweka msingi wa utekelezaji wa sera za taifa za uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu, huku Ukerewe ikitajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuunganisha uhifadhi na maendeleo ya kiuchumi.