
16
Jun
Mambo saba yaliyoibeba TFS kuchangia Sh. bilioni 29.8
- Yaja na vipaumbele vitano kusalia kileleni
MIONGONI mwa habari kubwa zinazogusa maisha ya Watanzania wengi wiki hii, ni uwasilishaji wa mapato katika mfuko mkuu wa serikali, uliofanywa na mashirika ya serikali na taasisi zinazotengeneza faida na zile zisizo za kibiashara, zilizotoa gawio la Sh. trilioni 1.28.
Kiasi hicho cha fedha, kitasaidia pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali, lakini pia kupunguza utegemezi wa serikali kwa wahisani na wadau wa maendeleo.
Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), ni miongoni mwa taasisi za serikali zilizotoa mchango wa Sh. bilioni 29.8, ikiwa ni kuiwezesha nchi kujinasua kwenye utegemezi.
Katika mahojiano maalumu na Kamshana wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, anaeleza kwa kina safari ya TFS kufikia kutoa mchango huo, licha ya kwamba ni taasisi isiyo ya kibiasahara.
SWALI: TFS ni taasisi isiyo ya kibiashara, lakini tumewaona kwenye siku ya Gawio, mnashiriki vipi kwenye siku hii muhimu?
JIBU: Kwa taasisi ambazo sio za kibiashara kama TFS, tunatoa mchango wa kisheria wa asilimia 15. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwa mgeni rasmi katika siku hii ya Gawio; na maelekezo yake mahsusi ambayo yametusaidia kuijenga taasisi yetu kiasi cha kuwa mchangiaji mzuri mwaka hadi mwaka.
Mchango wa TFS kwenye serikali kwa upande wa taasisi zisizo za kibiashara, umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka jana tulitoa mchango wa Sh. bilioni 20, lakini mwaka huu tumepanda kufikia Sh. bilioni 29.8.
Jambo hili halijatokea hivi hivi, kama mnavyofahamu, serikali imewekeza, na uwekezaji katika sekta ya misiti ni kwamba serikali ina misitu yake ambayo sisi kama TFS tumepewa dhamana ya kuisimamia na kuiendeleza.
Uwekezaji mwingine uliofanyika ni rasilimali watu ambao serikali inawaajiri na sisi tunawasimamia; watumishi wetu wanafanyakazi kwa weledi, kwa kujituma na tunahakikisha wanapata mafunzo stahiki kuandaliwa vya kutosha kifikra ili watoe mchango wao wa kitaaluma kwa maendeleo ya taasisi.
SWALI: TFS inasimamia misitu yenye ukubwa gani na vyanzo vyake vya mapato vimegawanyika vipi?
JIBU: Wakala unasimamia hifadhi za misitu zipatazo 465 zenye jumla ya ukubwa wa hekta milioni 14.5. Pamoja na jukumu la msingi la usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki, TFS imekasimiwa jukumu la kukusanya na kusimamia mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali katika hifadhi hizi.
Mgawanyo wa vyanzo vikuu vya mapato umegawanyika katika maeneo sita, ambayo ni mapato yatokanayo na uuzaji wa magogo kutoka mashamba ya kupandwa yanayochangia asilimia 50.
Eneo la pili ni mapato yatokanayo na uuzaji wa magogo kutoka misitu ya asili yanayochangia asilimia 40 ya mapato yetu na la tatu ni yale yanayotokana na huduma mbalimbali za usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki.
Hapa kuna usajili na usafirishaji wa ndani na nje wa mazao ya misitu yanayochangia takribani asilimia tano ya jumla ya mapato.
Mapato mengine ni yanayotokana na huduma za utalii ikolojia na utamaduni yanayochangia asilimia mbili, uuzaji wa miche na vipande unatupatia asilimia moja na vyanzo vinginevyo kama vile uchimbaji wa madini, yanayochangia takribani mbili ya mapato yetu.
SWALI: Vipi Kuhusu ukusanyaji wa mapato, nini hasa vyanzo vya TFS, ikiwa sio taasisi ya kibiashara?
JIBU: Katika eneo la kukusanya mapato, TFS tunakusanya mapato kwa sehemu kubwa kutoka kwenye vyanzo vyetu ambavyo ni endelevu; hususani mashamba ya miti ambayo tunafanya kilimo cha miti kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa za mazao ya misitu nchini na kueneza viwanda.
Pia tuna eneo la nyuki, utalii na huduma mbalimbali ambazo zinapatikana katika misitu yetu.
Kwa hiyo mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji ambao tumeufanya kwenye maeneo hayo mahsusi.
Katika kusimamia rasimali za misitu na nyuki, tumefanikiwa kuongeza makusanyo ya maduhuli kwa wastani wa asilimia tisa kwa mwaka. Mfano, mwaka 2023/24, TFS ilifikia malengo kwa kukusanya mapato ya Sh. bilioni 165 sawa na 102 ya makisio ya mwaka.
Makusanyo katika kipindi hicho yaliongezeka kwa Sh. bilioni 21, sawa na ongezeko la asilimia 14.5, ukilinganisha na makusanyo halisi ya mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa mwaka huu wa fedha 2024/25, hadi Jumanne wiki hii (Juni 10), Wakala umekusanya Sh. bilioni 174.8 sawa na asilimia 99 ya masikio ya mwaka. Makusanyo hadi tarehe hiyo yameongezeka kwa Sh. bilioni 10 sawa na ongezeko la asilimia sita, ukilinganisha na makusanyo halisi ya mwaka wa fedha 2023/24.
SWALI: Nini tafsiri ya ongezeko hili la mapato kwa Mtanzania mmoja mmoja?
JIBU: Ongezeko hili limeongeza mchango wa TFS kwenda Mfuko Mkuu-Hazina, ambao kwa bajeti ya serikali, unagusa sekta zote kama afya, elimu, miundombinu, nishati, kilimo na nyinginezo. Kwa hiyo kama kuna vijiji vitapelekewa umeme, TFS ina mkono wake.
Ongezeko hili limeongeza, mchango wa TFS kwenda Mfuko Mkuu kutoka Sh. bilioni 25.54 mwaka 2023/24 hadi kufikia Sh. bilioni 29.82 mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 16.75.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Wakala ushawasilisha kwenye mfuko huo, jumla ya Sh. bilioni 74.24. Mafanikio haya yameiwezesha Wakala kushika nafasi ya tatu kwa miaka miwili mfululizo kwa Taasisi zinazochangia asilimia 15 kwenda Mfuko Mkuu.
SWALI: Ni kwa namna gani TFS inashirikiana na taasisi nyingine za serikali katika kufikia malengo yake?
JIBU: Namna ambavyo tunashirikiana na taasisi nyingine za serikali kwenye usimamizi wa rasilimali za misitu imeongeza tija sana. Kwa mfano, kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), tumeshirikiana na mamlaka husika ambayo imetusaidia sana kujenga mifumo thabiti ya kusimamia makusanyo ya mapato ya serikali na matumizi yake.
Uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA imetusaidia sana kutoa huduma kwa haraka na kwa uhakika.
SWALI: Kuna eneo lingine mahsusi ambalo TFS imepeleka nguvu na sasa tunaona matokeo?
JIBU: Eneo ambalo tumefanya uwekezaji wa kimkakati ni kwenye kuendeleza mazao yale ambayo hayakuwa ya kitamaduni kwa sekta ya misitu hususani utalii. Maeneo haya tumewekeza sana hasa miundombinu ya kuwezesha shughuli za utalii kwenye misitu na kuongeza wigo wa huduma za kitalii.
Mfano, utalii wa michezo. Tumewekeza sasa hivi utaona kuna mbio za magari kwenye misitu, kwenye misitu yenye mabwawa, kuna utalii wa boti na kupiga makasia, yote haya yanaisaidia TFS kutoa huduma kwa jamii, lakini kukusanya pia mapato kwa njia endelevu. Hili limetuwezesha kuwa na mapato yanayoongezeka mwaka hadi mwaka.
Tunajivunia kuona ongezeko la mapato ghafi tunayokusanya. Kwa wastani, mapato ghafi ya TFS yanaongezeka kwa asilimia tisa kila mwaka. Kwa sababu ya ubunifu tunaouweka, watumishi wanavyojituma na namna ambavyo tunaelekeza na kubana matumizi. Kingine kinachochangia ongezeko hili ni matumizi ya teknolojia katika kazi zetu.
SWALI: Nini siri ya mapato ya TFS kuongezeka mwaka hadi mwaka?
JIBU: Jambo la kwanza ni matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki pamoja na ukusanyaji wa mapato.
La pili, ni kuongeza upandaji wa miti katika mashamba ya kupandwa. Wakala unapanda wastani wa hekta 10,000 kwa mwaka. Tumefanya pia ukaguzi madhubuti wa usafirishaji wa mazao ya misitu na nyuki.
Pia tumefanya mabadiliko ya mifumo ya kiutendaji, uwekezaji katika miundombinu ya utalii, tumebuni mazao mapya, ukiwamo uvunaji wa utomvu na ujenzi wa miundombinu katika hifadhi za misitu.
SWALI: Ni kwa namna gani TFS imejipanga kubakia kwenye nafasi yake katika kuwahudumia Watanzania kupitia mchango wake kwenye mfuko mkuu?
JIBU: Kwanza, wakala utatanua wigo wake wa upandaji katika mashamba ya miti ya kupandwa.
Tutatumia fursa ya biashara ya kaboni, tutaendelea kujenga mazingira rafiki kwa wawekezaji wa viwanda vya misitu nchini na kuboresha mifumo ya usimamizi wa rasilimali za misitu.
Pia, tutaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato. Tunaamini hatua hizi, zitausaidia Wakala kuendelea kuongeza usimamizi wa rasilimali za misitu, kuongeza makusanyo ya mapato yake na kuongeza uwasilisha wa mchango kwenda Mfuko Mkuu.