21
Mar

Serikali Yaendelea Kuweka Mazingira Wezeshi kwa Uwekezaji wa Sekta ya Misitu

Njombe, 21 Machi 2025 – Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha sekta ya misitu inachangia kikamilifu maendeleo ya taifa kwa kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali hii muhimu.

Akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika mkoani Njombe, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya misitu kuongeza thamani ya mazao ya misitu hapa nchini badala ya kusafirisha malighafi nje ya nchi.

“Tanzania ina teknolojia ya kutosha kwa uchakataji wa mazao ya misitu na utengenezaji wa samani. Hakuna sababu ya kusafirisha malighafi nje ya nchi kwa ajili ya uchakataji. Ni lazima tuweke ukomo wa uvunaji na kuhakikisha kila kitu kinafanyika hapa nchini, kama inavyofanywa na TANWAT,” amesema Mhe. Majaliwa.

 

Katika kuhakikisha sekta ya misitu inachangia uchumi wa taifa kwa ufanisi, Mhe. Majaliwa ameielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika mashamba ya miti na viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu. Aidha, amesisitiza umuhimu wa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa misitu na fursa za biashara ya kaboni, ili kuwawezesha kunufaika kiuchumi kupitia sekta hiyo.

Katika kupambana na changamoto ya uchomaji moto hovyo kwenye misitu, Mhe. Majaliwa amezitaka taasisi za misitu kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ya ufuatiliaji na udhibiti wa moto. Pia amezihimiza wizara na taasisi husika kuboresha ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa sekta ya misitu na jamii zinazozunguka maeneo ya misitu, ili kuhakikisha mipango ya uhifadhi inatekelezwa kwa ufanisi.

Akiwa katika mkoa wa Njombe, Mhe. Majaliwa alitembelea kiwanda cha uchakataji wa mazao ya misitu cha TANWAT (Tanganyika Wattle Company Limited) ambapo alishuhudia hatua mbalimbali za uchakataji wa mazao ya misitu na uongezaji wa thamani ndani ya nchi.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mwaka Huu:"Ongeza thamani ya mazao ya misitu kwa uendelevu wa rasilimali kwa kizazi hiki na kijacho.”