13
Mar

MHIFADHI MKUU WINO AWATAKA WATUMISHI KUSIMAMA IMARA KUTIMIZA MAELNGO YA TAASISI

Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Wino, SCO Glory Kasmir, amewataka watumishi wa shamba hilo kusimama imara na kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji ili kuhakikisha vipaumbele na malengo ya taasisi yanafikiwa kwa ufanisi.

Kasmir ametoa wito huo wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika ofisi za shamba hilo, kikilenga kupima utendaji kazi na maendeleo ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.

Amesema vikao vya tathmini vina umuhimu mkubwa katika kuimarisha utendaji kazi kwa kuwa vinatoa fursa kwa watumishi kujadili mafanikio yaliyopatikana, kubaini changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utekelezaji wa majukumu katika kipindi kinachofuata.

“Ni muhimu kila mtumishi kusimama imara katika nafasi yake na kutekeleza majukumu kwa weledi, huku akizingatia uwajibikaji na kulinda mali za Serikali ili kuendelea kuboresha utendaji wa taasisi,” amesema Kasmir.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na nidhamu ya kazi miongoni mwa watumishi ili kuhakikisha shughuli za uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za misitu zinafanyika kwa ufanisi na tija.

Katika kikao hicho, baadhi ya watumishi waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizofanyika katika robo ya tatu, wakieleza hatua zilizofikiwa pamoja na mipango ya kuendeleza shughuli hizo katika kipindi kijacho.