12
Mar
DC MOSHI AFUNGUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI,MICHE 4900 YAPANDWA SANGITI
Na Mwandishi Wetu, Moshi
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Eliakimu Mnzava, amezindua rasmi kampeni ya upandaji miti wilayani humo huku miche 4,900 ikipandwa na kugawiwa kwa wananchi katika Shule ya Sekondari Sangiti na maeneo yanayoizunguka, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Kupanda Miti yatakayofanyika kitaifa Machi 21, 2026.
Uzinduzi huo uliofanyika Leo Machi 12, 2026, umeandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Moshi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mnzava aliipongeza TFS kwa juhudi zake za kulinda rasilimali za misitu kupitia utoaji wa elimu kwa umma, usimamizi wa sheria za misitu pamoja na kugawa na kupanda miche ya miti katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
“Hii ni kazi kubwa mnayoifanya kuhakikisha mazingira yetu yanabaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi za uhifadhi wa misitu na mazingira,” alisema Mhe. Mnzava.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji na kata kusimamia ipasavyo miche yote ya miti inayopandwa katika maeneo yao ili kuhakikisha inakua na kufikia malengo ya uhifadhi.
Aliagiza pia hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu wanaoharibu mazingira kwa kukata miti bila vibali, kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi na maeneo yaliyopandwa miti, pamoja na wale wanaochoma moto ovyo katika misitu.
“Viongozi wa maeneo mhakikishe mnalinda miti inayopandwa. Pia wachukuliwe hatua wale wote wanaohusika na vitendo vya uharibifu wa misitu,” alisisitiza.
Mhe. Mnzava aliwahamasisha wananchi wa Moshi na Watanzania kwa ujumla kuungana na Serikali katika kampeni ya kupanda miti, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa TFS kutoka Wilaya ya Moshi, Zayana Mrisho, alisema katika msimu wa masika wa mwaka 2026 wilaya hiyo imelenga kupanda jumla ya miche 100,000 katika maeneo mbalimbali ikiwemo hifadhi za misitu, vyanzo vya maji, taasisi za umma na maeneo binafsi ya wananchi.
Alisema lengo hilo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uoto wa asili na kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, Mrisho alibainisha kuwa juhudi za uhifadhi bado zinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukataji miti bila vibali, baadhi ya wananchi kutunza vibaya miche wanayogawiwa hali inayosababisha kufa kabla au baada ya kupandwa, pamoja na mifugo kuingia katika maeneo ya uhifadhi na yale yaliyopandwa miti.
Kutokana na changamoto hizo, aliwataka wananchi kushirikiana na taasisi za uhifadhi katika kulinda rasilimali za misitu ili kuhakikisha juhudi za upandaji miti zinafanikiwa.
Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya, kata na vijiji pamoja na wanafunzi na wananchi wa maeneo ya jirani waliojitokeza kushiriki zoezi la kupanda miti.
Kitaifa, maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Kupanda Miti mwaka huu yanatarajiwa kufanyika mkoani Lindi, yakilenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa misitu na mazingira kwa kupanda mit