15
May
WATALII WAONGEZEKA KWA ASILIMIA 20 KATIKA MISITU YA HIFADHI YA TFS
Mapato yavuka Sh bilioni 3 huku matamasha ya misitu yakivutia maelfu
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
IDADI ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii ikolojia vinavyosimamiwa na TFS imeongezeka kwa asilimia 20 katika mwaka mmoja, ikionyesha kukua kwa utalii wa mazingira nchini.
Akizungumza wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2026/2027 Mei 15, 2026 bungeni Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii (Mb), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alisema watalii 329,753 walitembelea vituo vya utalii ikolojia hadi Aprili 2026 kutoka watalii 275,723 katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kutokana na ongezeko hilo, mapato ya utalii yamefikia Sh bilioni 3.09 kutoka Sh bilioni 2.16 mwaka uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 43.
Katika kuimarisha sekta hiyo, TFS imejenga malango sita ya utalii katika maeneo mbalimbali yakiwemo Meru, Vikindu, Mlima Rungwe na Ziwa Duluti.
Pia imekarabati kilomita 287.14 za njia za watembea kwa miguu, barabara za ndani ya misitu pamoja na kambi nane za watalii.
Matamasha ya utalii na michezo ya mazingira yaliyofanyika mwaka huu ni pamoja na “Tukutane Mt. Rungwe Season II”, “Lake Ngosi”, “Meru Adventure Race” na “Kalambo Waterfalls Utalii Festival”.
Katika mwaka 2026/2027, TFS imepanga kuimarisha miundombinu ya utalii kuelekea matukio makubwa ya kimataifa ikiwemo AFCON na Miss World.
𝐓𝐚𝐤𝐰𝐢𝐦𝐮 𝐳𝐚 𝐔𝐭𝐚𝐥𝐢i
* Watalii 2025/26: 329,753
* Watalii 2024/25: 275,723
* Ongezeko: 20%
* Mapato 2025/26: Sh bilioni 3.09
* Ongezeko la mapato: 43%