13
Mar
SAO HILL YAKAGUA UTEKELEZAJI WA KAZI ROBO YA TATU
Iringa, Machi 13, 2026 — Shamba la Miti Sao Hill linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) limefanya ukaguzi wa utekelezaji wa kazi kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayolenga kufuatilia utekelezaji wa mpango kazi na kubaini changamoto ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
Ukaguzi huo uliongozwa na Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill anayeshughulikia Mipango, Matumizi na Masoko ya Rasilimali Misitu, Peter Nyahende, aliyeshirikiana na wahifadhi wengine kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji na utendaji kazi ndani ya shamba hilo lililopo Sao Hill Forest Plantation.
Katika ukaguzi huo, timu ya tathmini ilikagua shughuli kadhaa ikiwemo bustani na vitalu vya miche ya miti vinavyoandaliwa kwa ajili ya msimu ujao wa upandaji miti, ujenzi wa barabara za kinga moto kwa lengo la kudhibiti na kupunguza matukio ya moto msituni, pamoja na usafishaji wa mashamba ya miti na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na mazao ya misitu.
Aidha, ukaguzi huo ulihusisha tathmini ya utendaji wa vitengo mbalimbali vya shamba hilo, vikiwemo Uvunaji na Leseni, Utawala, Ulinzi wa Msitu, Ugani na Uenezi, Utalii, Ujenzi na Barabara, Karakana pamoja na shughuli za ufugaji nyuki na uchakataji wa mazao yake.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Nyahende aliwataka watumishi wa shamba hilo kuendelea kuzingatia mpango kazi wa mwaka na kuutekeleza kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyowekwa na taasisi.
Alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ushirikiano na ubunifu kazini ili kuongeza tija katika shughuli za uhifadhi na uzalishaji wa rasilimali misitu.
Pia alieleza kuwa ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya shamba na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayolizunguka, akisisitiza kuwa jamii hizo ni wadau muhimu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali misitu