13
Feb

ZANZIBAR YAPONGEZA MAPINDUZI YA TFS MANYONI SEKTA YA NYUKI

Uzalishaji wa asali waruka mara tatu kwa miaka mitatu

Manyoni: Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Manyoni kwa kuimarisha usimamizi wa shughuli za ufugaji nyuki, hatua iliyochochea ongezeko kubwa la uzalishaji wa asali na nta pamoja na kuinua biashara ya mazao hayo kwa jamii.

Pongezi hizo amezitoa jana Februari 12, 2026 baada ya kupokea wasilisho la hali ya uzalishaji wa asali na nta kwa kipindi cha miaka mitatu (2022/2023–2024/2025) lililotolewa na Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Nyuki Manyoni, Igunda John, ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo ya wataalamu kutoka Zanzibar.

Takwimu zilizowasilishwa zinaonyesha kuwa uzalishaji wa asali umeongezeka kutoka kilo 4,992.6 mwaka 2022/2023 hadi kilo 14,665.7 mwaka 2024/2025, huku uzalishaji wa nta ukipanda kutoka kilo 159.8 hadi kilo 489 katika kipindi hicho — ongezeko linalokaribia mara tatu ndani ya miaka mitatu.

Akizungumza baada ya wasilisho hilo, Said alisema mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa elimu kwa jamii na usimamizi madhubuti wa mnyororo mzima wa thamani kuanzia shambani hadi kwenye uchakataji.

“Ni dhahiri TFS Manyoni mmefanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii kuhusu faida za kufuata kanuni bora za ufugaji nyuki. Hapo awali wengi hawakutambua thamani ya mazao ya nyuki, lakini sasa mwitikio ni mkubwa na wananchi wameanza kunufaika kiuchumi,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka wataalamu waendelee kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu, hususan kuhusu namna ya kutambua ubora wa asali na mazao mengine ya nyuki ili kulinda afya za watumiaji na kukuza soko la bidhaa halali.

Kwa upande wake, Igunda alisema ongezeko hilo limetokana na kubaini na kushughulikia changamoto katika uzalishaji na uchakataji, sambamba na kuimarisha mafunzo kwa wafugaji. Alisema baadhi ya wananchi sasa wamepanua shughuli zao na kuwa wafanyabiashara wakubwa wa mazao ya nyuki.

Katika siku ya pili ya ziara yao, wataalamu kutoka Idara ya Misitu Zanzibar walitembelea Hifadhi ya Nyuki Aghondi na kujionea mifumo ya kisasa ya ufugaji, kabla ya kupata mafunzo ya uchakataji katika Kiwanda cha TFS Manyoni kinachoongeza thamani ya mazao hayo.

Ziara hiyo ya siku tano inalenga kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na TFS Bara katika kukuza sekta ya nyuki kama chanzo cha ajira, mapato na nyenzo muhimu ya uhifadhi wa misitu.