01
Nov

MBUNGE KILINDI AFURAHISHWA NA JUHUDI ZA TFS ZA KUHIFADHI MISITU.

Mbunge wa Kilindi Mh. Swalehe Mbwana Mhando ameridhishwa na kufurahishwa na juhudi za TFS katika kuhifadhi misitu na kutoa huduma kwa wananchi!
Pongezi hizo alizitoa jana tarehe 31 Oktoba, 2026 wakati wa kikao kifupi kati ya Kamanda wa Kanda na Mbunge huyo kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilindi.

Mh. Mhando pia aliipongeza TFS kwa juhudi za kuchangia maendeleo ya jamii kufuatia mchango wa TFS wa Sh. Milioni 50 zilizojenga nyumba ya Walimu katika Shule ya Msingi na Awali Bondo pamoja na mbao 200 zilitolewa katika kijiji hicho kinachopakana na hifadhi ya msitu wa Bondo.

Pamoja na pongezi hizo Mbunge huyo aliiomba TFS mambo manne ambayo ni-;
1. Kuanzisha Shamba la Miti katika hifadhi ya Bondo ambayo ilikombolewa kutoka katika uvamizi kwa kuwaondoa wananchi,l.

2. Kujenga Ofisi ya TFS wilaya ya Kilindi katika kijiji cha Kwediboma badala ya  mji wa Songe ambapo makao makuu ya wilaya yapo.
3. Kuchangia madawati katika shule mbali mbali wilayani humo ambapo alisema yanahitajika madawati 4,000.
4. TFS kuingiza misitu ya wilayani Kilindi katika biashara ya hewa ukaa (Carbon trade).

Akipokea maombi hayo, kwa niaba ya Kamanda wa Kanda, PCO I Pamela Kessy alimweleza Mh. Mbunge kuwa kuhusu suala la  kuanzisha Shamba, TFS imeshafanya hatua za awali za kufanya tathmini ya rasilimali za msitu huo na hivyo ombi lake na matokeo ya tathmini hiyo vitapelekwa kwa Mkuu wa Taasisi kwa kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa maamuzi.

Aidha, kuhusu Madawati, PCO Kessy alimweleza mbunge utaratibu wa kupata mbao kupitia misitu ya vijiji kwa kuwa TFS hatuvuni mbao katika misitu ya asili, hivyo utaratibu ufanyike ili shule zipate madawati. Hata hivyo alimweleza Mh. Mbunge kuwa Ofisi ya DAS kwa kushirikiana na DED wafanye tathmini ya mahitaji ya madawati katika shule moja yenye changamoto kubwa ya Makasini ili TFS kupitia bajeti zake za ndani iweze kuchangia, lakini sio kumaliza tatizo.

Pia, PCO Kessy alimweleza Mh. Mbunge kuwa suala la kuhamisha Shule ya Dolosenta iliyopo hifadhini Bondo baada ya watu kuondolewa, limefikia hatua nzuri ambapo Ofisi ya Mkurugenzi imeshatenga eneo nje ya hifadhi kwa ajili ya ujenzi wa Shule hiyo. Pia TFS imeshawasilisha andiko Mfuko wa Misitu Tanzania kuomba fedha za ujenzi wa shule hiyo.


Mwakilishi wa ZCC PCO Kessy pia alimhakikishia Mh. Mbunge kuwa maombi yake yote yamechukuliwa, yatajadiliwa kwenye menejiment ya Kanda na kupelekwa kwenye mamlaka husika za maamuzi.

Akiongezea, SCO Augustine Mugenyi ambaye ni msaidizi wa ZCC Kitengo cha Usimamizi wa Rasilimali alishauri kuundwa kwa kamati ya kusimamia upatikanaji wa mbao na madawati kutoka misitu ya vijiji ili kudhibiti uvunaji holela.

Baada ya kupata mrejesho wa ZCC, Mh. Mbunge aliahidi kuwa  atawasiliana na  Mfuko wa Misitu ili kuharakisha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa Shule. Pia aliahidi atasaidia kuhakikisha TFS inapata nyaraka na kurasimisha Ardhi waliyopewa Kwediboma ili kujenga Ofisi.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Wahifadhi kutoka wilaya Kilindi wakiongozwa na SCO Lais Lucumay, Kaimu Katibu Tawala (DAS) wilaya ya Kilindi na Katibu wa Mbunge.

Akihitimisha kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala wa wilaya Dr. Michael John alimweleza Mh. Mbunge kuwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya itashirikiana na TFS kuhakikisha suala la madawati linashughulikiwa ikiwemo kuratibu uundaji wa Kamati ya kusimamia upatikanaji wa mbao kupitia misitu ya vijiji, pamoja na kusaidia kurasimisha eneo walilopewa TFS katika kijiji cha Kwediboma ili kujenga Ofisi ya Mhifadhi Misitu wa Wilaya (DFC).