17
Nov

TFS YATWAA MEDALI TISA, YAONGOZA RIADHA SHIMMUTA 2026

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeibuka kinara katika mchezo wa riadha kwenye mashindano ya SHIMMUTA 2026 baada ya wanariadha wake kutwaa jumla ya medali tisa, zikiwemo nafasi za kwanza katika mbio za mtu mmoja mmoja na za kupokezana vijiti.

Mafanikio hayo yaliyopatikana katika mashindano yaliyofanyika Novemba 17 na 18, mwaka huu, katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, yameifanya TFS kuwa taasisi iliyotwaa medali nyingi zaidi katika mchezo huo ikilinganishwa na taasisi nyingine zilizoshiriki.

Katika mafanikio hayo, Eunice Makondo alikuwa miongoni mwa vinara wa ushindi baada ya kutwaa medali mbili za dhahabu katika mbio za mita 200 na 800, huku Ester Mwaifani akiipa TFS medali nyingine ya dhahabu baada ya kushinda mbio za mita 100.

Kwa upande wa wanaume, Michael Kalayi alitwaa medali tatu za fedha baada ya kushika nafasi ya pili katika mbio za mita 5,000, 1,500 na 800, huku Dorothea Lyambi akiongeza medali nyingine ya fedha kwa kushika nafasi ya pili katika mbio za mita 800.

Katika mbio za kupokezana vijiti, timu ya wanawake ya TFS ilitwaa nafasi ya kwanza na kupata medali ya dhahabu, wakati timu ya wanaume ikishika nafasi ya pili na kuongeza medali nyingine ya fedha.

Wakizungumza na Forest TV, kwa nyakati tofauti, wanariadha hao walisema mafanikio hayo yametokana na maandalizi, kujituma na kufanya mazoezi kwa bidii, kumtanguliza Mungu katika kila hatua pamoja na kuzingatia maelekezo ya viongozi wao.

Aidha, waliishukuru menejimenti ya TFS chini ya Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo, kwa kuwaunga mkono na kuwapatia mazingira ya kushiriki mashindano hayo, wakiahidi kuendeleza kiwango hicho na kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.

Ushindi huo unaonesha mchango wa TFS katika kukuza michezo na vipaji miongoni mwa watumishi wake, sambamba na kujenga afya, mshikamano, nidhamu na ari ya utendaji kazi ndani ya taasisi.