22
Nov
TFS YATWAA VIKOMBE VITATU SHIMUTA 2026
Timu ya michezo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imefanya vizuri katika Mashindano ya SHIMUTA 2026 yaliyofanyika mjini Morogoro kuanzia Novemba 6 hadi 21, 2026, kwa kutwaa vikombe vitatu katika michezo mbalimbali.
Katika mashindano hayo, TFS imeibuka mshindi wa kwanza kwa jumla katika riadha, mshindi wa tatu katika netiboli na mshindi wa tatu katika mchezo wa baiskeli.
Mashindano ya SHIMUTA 2026, yaliyoandaliwa na Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania, yalishirikisha zaidi ya wanamichezo 5,000 kutoka timu zaidi ya 700 zilizoshindana katika michezo 12.
Mashindano hayo yalikuwa na kaulimbiu “Michezo Ituunganishe Kuelekea AFCON 2027,” yakilenga kuimarisha mshikamano, afya, ushirikiano na kuhamasisha maandalizi kuelekea mashindano ya AFCON 2027.
Mafanikio ya TFS yanaonesha juhudi, nidhamu na uwezo wa wanamichezo wake, ambao wameitendea haki taasisi kwa ushindani na kuonesha umahiri katika michezo waliyoshiriki.
Akizungumza mara baada ya kutamatika kwa mashindano hayo Mrakibu wa Michezo TFS, Mhifadhi Mwandamizi. SCO Marcel Bitulo, amempongeza Kamishna kwa kuwaamini wanamichezo hao na kuwapa nafasi ya kuiwakilisha taasisi katika mashindano hayo.
SCO Bitulo amesema mafanikio yaliyopatikana ni chachu ya kuimarisha maandalizi na kuongeza ari ya ushindani katika mashindano yajayo, akieleza kuwa TFS imejipanga kufanya vizuri zaidi mwaka ujao.
“Mwaka ujao tumejipanga kushinda katika kila mchezo, kutwaa vikombe na medali katika michezo yote tutakayoshiriki,” amesema Bitulo.
TFS inaendelea kutumia michezo kama sehemu ya kuimarisha afya, mshikamano, nidhamu na morali ya watumishi, sambamba na kujenga taswira chanya ya taasisi.