24
Nov

EU YAVUTIWA NA UHIFADHI WA MIKOKO, UTALII WA BAHARI UNAOFANYWA NA TF


Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Jean-Marc Pisani, amevutiwa na juhudi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika uhifadhi wa mikoko na kuendeleza utalii wa bahari unaochangia kukuza uchumi wa buluu.

Balozi Pisani ameeleza kuvutiwa kwake Novemba 24, 2026, wakati ujumbe wa Umoja wa Ulaya ulipotembelea daraja la mikoko (Mangrove Boardwalk) jijini Tanga, kujionea shughuli za uhifadhi na fursa za utalii zinazotokana na rasilimali za bahari.

Amesema Umoja wa Ulaya unatambua juhudi za TFS katika uhifadhi wa mikoko, ambayo ina mchango mkubwa katika kulinda bioanuai, kuhifadhi mifumo ikolojia ya bahari na kukinga maeneo ya pwani dhidi ya mmomonyoko.

“Tunatambua jitihada zinazofanywa na TFS katika uhifadhi wa mazingira, hasa maeneo ya bahari ambayo ni muhimu kwa uchumi wa buluu,” amesema Pisani.

Ameongeza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kutambua fursa za ushirikiano kati ya EU na TFS katika kulinda rasilimali za bahari na kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazotokana nazo kwa kuzingatia matumizi endelevu.

“Moja ya agenda iliyotuleta ni kuona namna ya kuendelea kushirikiana na TFS katika kutambua fursa za kiuchumi, huku lengo letu kuu likiwa kulinda na kuhifadhi fukwe za bahari,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Rasilimali za Misitu wa TFS, Dkt. Elkana John, amesema uchumi wa buluu ni fursa muhimu ya kuongeza thamani ya rasilimali za maji, kukuza utalii wa baharini na kuimarisha shughuli za kiuchumi zinazotegemea rasilimali hizo.

Amesema ziara hiyo imelenga pia kubadilishana uzoefu kuhusu umuhimu wa mikoko katika kuhifadhi bioanuai, kusaidia shughuli za uvuvi, kulinda maeneo ya pwani na kutambua fursa zinazoweza kuchochea maendeleo ya jamii kupitia uchumi wa buluu