20
Nov
DKT. MUSHUMBUSI: TEKNOLOJIA ZA KISASA ZILETE TIJA KATIKA UHIFADHI WA MISITU
Na Mwandishi Wetu, Iringa
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dkt. Revocatus Mushumbusi, amewataka washiriki wa mafunzo ya teknolojia za kisasa kutumia ujuzi walioupata kuleta matokeo halisi katika uhifadhi na usimamizi wa misitu nchini.
Akifunga mafunzo hayo Novemba 20, 2026, katika Shamba la Miti Sao Hill, Iringa, Dkt. Mushumbusi amesema Serikali inatarajia teknolojia hizo zitumike kuboresha utendaji kazi, kutambua changamoto mapema na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za misitu.
“Tunatarajia kuona mabadiliko katika utendaji kazi. Maarifa na ujuzi tulioupata lazima ulete tija katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu,” amesema.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Novemba 18 hadi 20, 2026, yalihusu matumizi ya teknolojia za kisasa katika ufuatiliaji, utambuzi wa mapema na udhibiti wa moto misituni, yakiwemo ndege zisizo na rubani (drones), akili mnemba (AI) na teknolojia za vihisishi vya mbali.
Dkt. Mushumbusi amewashukuru washirika kutoka Urusi, akiwemo Geoscan Group of Companies, Peter the Great Botanical Garden na Chuo Kikuu cha Ufundi wa Umeme cha Saint Petersburg (LETI), kwa mchango wao wa kitaalamu na kiteknolojia katika kufanikisha mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ujumbe wa Urusi na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Umma wa Misaada wa Saint Petersburg, Vladimir Kulgaviy, amesema matumizi ya teknolojia hizo yataimarisha utambuzi wa mapema wa changamoto za misitu na kuwezesha hatua za haraka katika kukabiliana nazo.