10
Nov
TANZANIA YAONESHA MAFANIKIO YA UFUGAJI NYUKI KATIKA UHIFADHI WA MISITU COP31
Antalya, Uturuki – Novemba 9, 2026
Tanzania imewasilisha mafanikio ya kutumia ufugaji nyuki endelevu, upandaji miti na matumizi ya nishati safi katika kuhifadhi misitu ya maeneo kame na kuboresha maisha ya wananchi, katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika jijini Antalya, Uturuki.
Mafanikio hayo yamewasilishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika mjadala wa kitaalamu ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Serikali ya Uturuki, uliolenga kubadilishana uzoefu kuhusu uhifadhi na urejeshaji wa mazingira katika maeneo kame.
Akiwasilisha mada yenye kichwa “Dryland Forest Conservation through Sustainable Beekeeping”, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa TFS, Fandey H. Mashimba, amesema ufugaji nyuki unaotegemea misitu unatoa motisha kwa jamii kulinda misitu badala ya kuitegemea kwa shughuli za kiuchumi zinazoweza kusababisha uharibifu.
Katika kuonesha matokeo ya utekelezaji, TFS imeeleza kuwa kupitia Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mazingira katika Misitu ya Miombo ya Maeneo Kame (DSL-IP), jumla ya mizinga 500 ya nyuki imegawiwa, huku bustani nane za miti ya matunda, kivuli na mbao zikiwa na uwezo wa kuzalisha miche takribani milioni nne. Aidha, majiko 600 ya nishati nafuu yamegawiwa ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Mradi huo pia umejenga majengo na kuweka vifaa vya uchakataji mbegu katika vituo vya mbegu vya miti vya Kaliua mkoani Tabora na Shinyanga, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa uzalishaji na uchakataji wa mbegu bora za miti kwa ajili ya upandaji na urejeshaji wa misitu.
Mradi huo unaotekelezwa katika wilaya za Kaliua, Urambo na Sikonge mkoani Tabora, pamoja na Mlele mkoani Katavi, unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF-7) kwa kushirikiana na FAO. Unalenga kuunganisha uhifadhi wa misitu na shughuli endelevu za kiuchumi, ikiwemo ufugaji nyuki, kilimo mseto, uzalishaji wa mbegu za miti na uimarishaji wa minyororo ya thamani ya mazao yatokanayo na misitu.
Ushiriki wa TFS katika COP31 ni sehemu ya juhudi za Tanzania kutangaza mafanikio yake katika uhifadhi wa mazingira, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.