17
Nov
TFS KUIMARISHA USIMAMIZI WA MISITU KWA TEKNOLOJIA, WAHIFADHI 40 KUPATIWA MAFUNZO
Na Mwandishi Wetu
Wahifadhi 40 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanatarajia kupatiwa mafunzo ya matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa misitu, hususan ufuatiliaji, utambuzi na udhibiti wa moto katika hifadhi.
Mafunzo hayo yatafanyika katika Shamba la Miti Sao Hill, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, kuanzia Novemba 17 hadi 21, 2026, yakitolewa na wataalamu 11 kutoka Urusi.
Akizungumza jijini Dodoma Novemba 17, 2026, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uwezo wa watumishi kutumia teknolojia za kisasa katika kulinda na kusimamia rasilimali za misitu.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yatajikita katika matumizi ya ndege nyuki (drone) pamoja na teknolojia za kisasa za kubaini na kudhibiti moto misituni.
Prof. Silayo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Urusi yaliyosainiwa Septemba 2025, ambapo TFS iliwakilisha upande wa Tanzania na Chuo Kikuu cha St. Petersburg upande wa Urusi.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo tayari umeanza kuzaa matunda, ambapo watumishi tisa wa TFS wanaendelea na masomo ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Misitu cha St. Petersburg nchini Urusi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utaongeza ujuzi na uwezo wa TFS kutumia teknolojia bunifu katika kuimarisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu nchini.