24
Sep
MAWAZIRI WATATU WAKUTANA NA WANANCHI KUSHUGHULIKIA MGOGORO WA MIPAKA PUGU
DAR ES SALAAM. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Profesa Riziki Shemdoe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande, wamekutana na wananchi wa maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Msitu wa Pugu–Kazimzumbwi kusikiliza malalamiko yao kuhusu mipaka ya hifadhi na mipaka ya kiutawala.
Kikao hicho kilichofanyika Dar es Salaam leo, Septemba 23, 2026, kimekuja siku chache baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, kuwaagiza mawaziri wenye dhamana ya TAMISEMI, Ardhi na Maliasili na Utalii kufika Pugu ndani ya siku saba na kushughulikia kero za wananchi kuhusu mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, viongozi waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na TFS Kanda ya Mashariki pamoja na viongozi na wataalamu kutoka taasisi na mamlaka mbalimbali zinazohusika na suala hilo.
Katika kikao hicho, wananchi waliwasilisha madai na hoja zao zinazohusu mpaka wa hifadhi pamoja na changamoto ya mpaka wa kiutawala kati ya Dar es Salaam na Pwani, hususan katika eneo la Zingiziwa.
Baada ya kusikiliza mawasilisho hayo, Mhe. Profesa Shemdoe aliiagiza timu ya wataalamu kuanza kushughulikia madai yaliyowasilishwa kwa haraka, kwa lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto hizo.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais yaliyotolewa Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu na kusikiliza kero za wananchi wanaoishi katika maeneo ya jirani. Katika maelekezo hayo, alisisitiza matumizi ya taarifa rasmi za Serikali kuhusu mipaka ya kiutawala, ikiwemo Government Notice (GN) iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali, kama msingi wa kubaini mipaka husika.