
20
Mar
KKKT Masasi na TFS Wazindua Kampeni ya Upandaji Miti Kuelekea Siku ya Misitu Duniani
Masasi, 16 Machi 2025 – Ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya Masasi wamezindua rasmi kampeni ya upandaji miti katika eneo la Kanisa la KKKT Masasi Mjini.
Katika uzinduzi huo, miti ya kivuli na matunda ilipandwa kuzunguka eneo la kanisa kama hatua ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuongeza thamani ya mazao ya misitu kwa maendeleo endelevu.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Lauteri Johni Kanoni, aliipongeza KKKT Masasi kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji wa miti. Alisisitiza kuwa miti ina mchango mkubwa kwa maisha ya binadamu na kutoa wito kwa taasisi nyingine za kidini na kijamii kuunga mkono juhudi hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jimbo la Magharibi (Masasi) la KKKT, Mchungaji Wayzimen Simwinga, aliwataka waumini na wananchi kwa ujumla kuheshimu uumbaji wa Mungu kwa kutunza miti. Alieleza kuwa miti ni chanzo cha hewa safi ya oksijeni na hivyo, ukataji miti holela unapaswa kudhibitiwa kwa kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.
Aidha, Mheshimiwa Kanoni aliipongeza TFS kwa mchango wake wa kugawa miche ya miti kwa wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa misitu.
Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Ijumaa, Machi 21, 2025, katika Uwanja wa Sabasaba, Halmashauri ya Njombe Mji, mkoani Njombe. Kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka huu ni:
“Ongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali kwa Kizazi Hiki na Kijacho.”
Kwa upande wa dunia, maadhimisho yanaongozwa na kauli mbiu: "Misitu na Chakula.”
Tukio hili linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa misitu na mchango wake katika usalama wa chakula, afya na maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.