
05
Jul
Kustaafu Utumishi wa Umma ni Kitendo cha Kishujaa — CP Wakulyamba
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba, amesema kustaafu utumishi wa umma ni kitendo cha kishujaa na cha kupongezwa.
Kamishna Wakulyamba alitoa kauli hiyo tarehe 4 Julai 2025, wakati wa hafla fupi ya kuwaaga Maafisa na Askari wa Uhifadhi waliostaafu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Mesuma, Area A, jijini Dodoma.
Akizungumza na wastaafu hao, Wakulyamba aliwapongeza kwa kulitumikia taifa kwa uadilifu na ujasiri, huku akiwashauri kuzingatia kanuni za maisha ya kustaafu, ikiwemo lishe bora na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kudumisha afya.
“Nawapongeza sana. Kustaafu utumishi wa umma ni kitendo cha kishujaa. Kati ya mambo ninayotaka kuwaambia ni kuishi kwa kufuata kanuni za maisha ya kustaafu, ikiwemo lishe bora na kufanya mazoezi mara kwa mara. Nimefurahi kuwaona wastaafu wengi hapa bado mna afya na nguvu. Hongereni sana,” alisema Wakulyamba.
Kamishna Wakulyamba pia aliuagiza Wakala wa Huduma za Misitu kuhakikisha wastaafu hao wanapatiwa mafao yao kwa wakati ili waweze kuendeleza maisha yao kwa utulivu na heshima baada ya utumishi wao.
Aidha, aliwahimiza Maafisa na Askari ambao bado hawajafikia muda wa kustaafu kujiandaa mapema, akisisitiza kwamba utumishi wa umma una kikomo na kwamba kustaafu siyo mwisho wa maisha.
Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alimshukuru Kamishna Wakulyamba kwa kukubali kuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo ya kuwaaga wahifadhi waliostaafu.
“Afande, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kukubali kuja kujumuika na makamanda hawa. Takribani Maafisa na Askari 57 waliostaafu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wataagwa leo,” alisema Prof. Silayo.
TFS imekuwa na utamaduni wa kutambua na kuthamini mchango wa watumishi waliostaafu kwa kuwaandalia hafla maalumu ya kuwaaga. Katika hafla hizo, wastaafu hukabidhiwa zawadi mbalimbali kama kumbukumbu ya utumishi wao wa uaminifu na kujitolea.