19
Feb
TFS YATAJWA ‘SLEEPING GIANT ‘WA UTALII- IKOLOGIA
TFS Yatajwa ‘Sleeping Giant’ wa Utalii-Ikolojia
Wakati Serikali ikilenga kuvutia watalii milioni tano na mapato ya dola za Marekani bilioni sita, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetajwa kuwa na uwezo wa kuwa mhimili mkuu wa kufanikisha azma hiyo kupitia utalii-ikolojia unaojali uhifadhi.
Hayo yameelezwa jana Februari 19, 2026 na Ibrahim A. Mussa, mstaafu aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Masoko katika TANAPA, wakati akiwasilisha mada kuhusu Fursa, Changamoto na Mwelekeo wa Utalii-Ikolojia TFS katika siku ya pili ya Mkutano wa Nne wa Viongozi na Makamanda wa Vituo vya TFS unaoendelea katika Ukumbi wa Hoteli ya Cate, Morogoro.
Mussa, aliyelitumikia sekta ya maliasili tangu mwaka 1982 katika ngazi mbalimbali ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema takwimu za miaka ya karibuni zinaonyesha ukuaji mkubwa wa utalii ndani ya hifadhi za misitu, akieleza kuwa TFS ni “sleeping giant” anayehitaji kuamshwa kimkakati.
Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, idadi ya wageni imeongezeka kutoka 59,606 mwaka 2020/21 hadi 152,954 katikati ya mwaka 2023/24, huku lengo la 2024/25 likiwa kufikia wageni 500,000. Mapato nayo yamepanda kutoka Sh154.9 milioni hadi Sh1.27 bilioni katika kipindi hicho, yakilenga kufikia Sh3 bilioni.
Alieleza kuwa mwelekeo wa dunia unahitaji taasisi kuondoka kwenye utegemezi wa mapato ya mbao na asali pekee na kuingia katika vyanzo jumuishi vinavyozingatia uhifadhi endelevu, matumizi endelevu ya rasilimali na ushirikishwaji wa wadau.
“Utalii-ikolojia si burudani tu; ni chombo cha kuimarisha uchumi wa kijani, kulinda bayoanuai na kufanya diplomasia ya uhifadhi,” alisema, akirejea mikakati ya TFS na sera ya taifa ya misitu.
Aliainisha fursa zilizofunguliwa na kanuni za Serikali ikiwemo Tangazo la Serikali Na. 132 la mwaka 2025 kuhusu burudani katika hifadhi za misitu pamoja na marekebisho ya kanuni za uwekezaji katika miundombinu ya utalii wa ikolojia, akisema zimeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kuwekeza kwenye eco-lodges na huduma rafiki kwa mazingira.
Miongoni mwa maeneo yenye mvuto aliyatolea mfano ni Amani Nature Reserve, Pugu-Kazimzumbwi Forest Reserve, Magamba Forest Reserve na Minziro Forest Reserve, akisisitiza kuwa yana sifa za kiikolojia zinazoweza kuvutia masoko maalum ya watalii wanaotafuta uzoefu wa asili usioharibiwa.
Hata hivyo, alionya juu ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo, zikiwemo mimea vamizi, athari za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya mipaka na shinikizo la kuongeza idadi ya watalii bila kupima athari kwa mifumo ya ikolojia.
“Ni rahisi kupima fedha na idadi ya wageni, lakini ni vigumu kupima mafanikio ya uhifadhi. Tusijikute tunaangukia mtego wa ‘niche trap’ bila kujua tupo daraja lipi la ubora wa utalii-ikolojia,” alisisitiza.
Katika mapendekezo yake, alitaka TFS iji-brand kama kinara wa utalii wa kijani, iboreshe ukusanyaji na uchakataji wa takwimu, itumie mbinu za kisasa za masoko zikiwemo segmentation na positioning, pamoja na kupanua matumizi ya teknolojia kama droni katika masoko na usalama wa watalii.
Pia alisisitiza umuhimu wa jamii za jirani kunufaika na miradi ya utalii ili kuimarisha ulinzi wa rasilimali, huku sekta binafsi ikipewa nafasi kubwa kuwekeza katika miundombinu badala ya taasisi kubeba mzigo mkubwa wa mtaji.
Wakizungumza pembeni mwa mkutano huo, baadhi ya viongozi wa TFS walisema mada hiyo imefungua mjadala mpana kuhusu namna ya kuoanisha malengo ya mapato na wajibu wa msingi wa uhifadhi.