25
Feb

BAJETI YA TFS 2026/2027 YALENGA KUENDELEZA MIRADI

Morogoro. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetangaza mkakati mkali wa kusimamia matumizi ya fedha na kukamilisha miradi iliyochelewa, katika bajeti yake ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 itakayotekelezwa chini ya Mpango Mkakati mpya wa nne wa taasisi.

Meneja wa Mipango na Masoko wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bi. Neema L. Mbise, amesema bajeti hiyo imejengwa kwa kuzingatia Sheria  za fedha za Umma, miongozo ya Serikali na vipaumbele vya Kitaifa, huku ikilenga kuondoa kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya nyuma.

Akizungumza katika kikao cha uchambuzi wa mpango na bajeti, Mbise alisema taasisi imejipanga kuhakikisha miradi ya maendeleo, hususan ya ujenzi, inakamilika kwa wakati baada ya kubainika kuwa baadhi ya miradi iliyopita haikukamilika kama ilivyopangwa.

Alisema bajeti ya mwaka ujao ndiyo ya kwanza kutekelezwa chini ya Mpango Mkakati wa Nne (ISP4) utakaotekelezwa hadi mwaka 2031, na kwamba fedha zote zitapangwa kwa kuzingatia malengo na viashiria mahsusi vya utekelezaji.

“Tunahakikisha kila fedha inayoombwa inaendana moja kwa moja na matokeo yanayotarajiwa. Hatutaki bajeti ya makaratasi, tunataka bajeti ya matokeo,” alisema.

Mbise alibainisha kuwa maandalizi hayo yamezingatia pia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu, ili kuendana na mwelekeo mpana wa Serikali.

Kwa mujibu wake, mwaka 2026/2027 utaweka mkazo katika maeneo manne: kuimarisha usimamizi wa misitu na nyuki kwa teknolojia ya kisasa, kuongeza mapato ya ndani, kukuza utalii wa misitu na kuimarisha uwezo wa taasisi kiutendaji.

Aidha, TFS imeanzisha mfumo wa kuwawajibisha wasimamizi wa vituo vya gharama ili kuhakikisha kila kitengo kinapanga na kutumia fedha kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa, hatua inayolenga kuongeza uwazi na kupunguza changamoto wakati wa ukaguzi.