06
Jul

Masauni: Tanzania Yazidi Kusonga Mbele Katika Mapambano ya Uharibifu wa Mazingira

Dar es Salaam, Julai 6, 2025 — Serikali imeahidi kuendelea kuchukua hatua thabiti kukabiliana na changamoto za kimazingira huku ikisisitiza umuhimu wa Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda misitu na afya za wananchi, hususan wanawake na watoto. 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, kupitia hotuba iliyosomwa na Katibu Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye Maonesho ya 49 ya Sabasaba.

Awali, Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dkt. Hamza Katete, aliongoza zoezi la upandaji miti na kubainisha kuwa TFS inaendelea kusaidia jamii kwa kugawa bure miche ya miti ya thamani kama mpingo na miti ya matunda aina ya stafeli, ili kuongeza uoto na kuboresha mazingira.

Dkt. Katete alisema kila mwaka Tanzania inapoteza zaidi ya hekta 469,000 za misitu, hivyo ni lazima juhudi za pamoja ziongezwe ili kufikia malengo ya kitaifa ya kila wilaya kupanda angalau miti milioni 1.5 kwa mwaka. 

Alibainisha kuwa TFS huzalisha wastani wa miche milioni 33 hadi 35 kila mwaka ambapo karibu nusu hupandwa kwenye mashamba ya Serikali na nyingine kugawiwa bure kwa wananchi, taasisi na watu binafsi.

Aidha, alieleza kuwa Wakala umeendelea kuanzisha maeneo ya utalii wa ikolojia katika misitu ya hifadhi kama Pugu Kazimzumbwi, Vikindu na Magamba Tanga, hatua inayolenga kuongeza thamani ya rasilimali na kuchochea uchumi wa kijani. Alisisitiza kuwa utalii wa ikolojia unakua kwa kasi huku juhudi pia zikielekezwa kulinda misitu ya vyanzo vya maji ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Masauni alisema kaulimbiu ya mwaka huu “Matumizi ya Nishati Safi na Uhifadhi wa Mazingira kwa Ustawi Bora wa Tanzania” inalenga kuhamasisha Watanzania kubadili mtindo wa maisha na kuachana na utegemezi wa kuni na mkaa unaoharibu misitu na kuathiri hewa safi. Alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya kaya nchini bado hutumia kuni na mkaa, jambo linaloleta madhara makubwa kiafya na kimazingira.

Masauni alisema Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) uliopo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na Rais Samia ameendelea kuwa balozi mkuu wa jitihada hizo.

Hata hivyo, Waziri Masauni alionya kuwa licha ya hatua zinazochukuliwa, Tanzania na dunia kwa ujumla bado zinakabiliwa na changamoto kama ukataji miti hovyo, uchafuzi wa hewa na maji, upotevu wa viumbe hai na taka za plastiki zinazoweza kuchukua hadi miaka 1,000 kuoza. Alitoa wito kwa wananchi kupunguza matumizi ya plastiki, kupanda miti na kutumia nishati mbadala ili kunufaika na biashara ya kaboni inayokua kwa kasi.

Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali imepiga marufuku mifuko ya plastiki na kuweka zuio la kuni na mkaa kwa taasisi kubwa huku ikihimiza uwekezaji wa sekta binafsi kwenye nishati safi. 

“Haturithi dunia kutoka kwa mababu zetu, bali tunaiazima kutoka kwa watoto wetu. Maamuzi tunayofanya leo yataunda Tanzania ya kesho,” alisema wakati akitangaza rasmi ufunguzi wa Siku ya Mazingira na Nishati Safi Sabasaba.