13
Jul

Nyuki Marathon Kufanyika Kesho AICC Club Arusha Kesho, Yalenga Kutangaza Ufugaji Nyuki Duniani

Arusha. Tanzania ipo tayari kutumia Nyuki Marathon itakayofanyika kesho kwenye viwanja vya AICC Club Arusha kama jukwaa la kuhamasisha ufugaji wa nyuki na maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 50 wa Apimondia unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha mwaka 2027.

Akizungumza na waandishi wa habari leo
Julai 12,2025 jijini Arusha, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Apimondia 2027, alisema kuwa mbio hizo zimekuwa chachu kubwa ya kutangaza umuhimu wa nyuki kwa usalama wa chakula na maendeleo endelevu ya wananchi.

“Mbio hizi zimeandaliwa mahususi kuhamasisha ufugaji wa nyuki na kutupa nafasi ya kujiandaa kama taifa kuwa mwenyeji wa kongamano kubwa duniani la nyuki. Ni mwaka wa pili sasa tunafanya mbio hizi, na kwa mara nyingine viongozi wa Apimondia duniani wameungana nasi,” alisema Prof. Silayo.

Ameongeza kuwa mbio hizo zinatoa fursa kwa Watanzania kutambua mchango wa nyuki katika uchumi na mazingira, kwani takribani asilimia 85 ya uzalishaji wa chakula duniani hutegemea uchavushaji unaofanywa na nyuki.

“Tunawaomba Watanzania , vijana, wazee, akina mama na watoto  wajitokeze kwa wingi. Ni ishara kwamba kama taifa tumeamua kulinda nyuki ambao wana mchango mkubwa kwenye usalama wa chakula na pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” aliongeza.

Prof. Silayo pia aliishukuru Serikali na wadau binafsi kwa kuunga mkono jitihada hizo, huku akiwakaribisha washiriki wote kwenye maandalizi ya kongamano la Apimondia 2027 litakalokutanisha wataalamu na wadau wa nyuki kutoka duniani kote.

Kwa upande wake, Rais wa Kamisheni ya Afrika ya Apimondia, Bw. David Mukomana, alisema kuwa Nyuki Marathon ni ishara ya Afrika kutambua umuhimu wa nyuki kama sehemu ya urithi wa bara na nyenzo ya kuimarisha usalama wa chakula na ajira.

“Afrika ni sehemu muhimu ya kijiji cha dunia. Kupitia nyuki tunaweza kuchangia mijadala ya kimataifa kuhusu amani, uhifadhi na maendeleo endelevu. Ni muda wetu kuthibitisha kuwa sekta hii inaweza kutoa ajira na kuondoa umasikini,” alisema Mukomana.

Alisisitiza umuhimu wa vijana na jamii kushiriki kama mabalozi wa nyuki na urithi wa Afrika, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya bara bado lina ardhi yenye rutuba inayoweza kuendeleza ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali bora duniani.

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Wafugaji Nyuki Duniani (Apimondia), Dk. Jeff Pettis, ameipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazouza asali nje ya nchi na kuonyesha uwezo mkubwa wa kukuza sekta hiyo.

“Tanzania ina historia nzuri kwenye ufugaji nyuki na ina nafasi kubwa ya kusonga mbele. Sekta hii inaweza kutoa ajira, kupunguza umasikini na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa nyuki ni viumbe muhimu kwa usalama wa mazingira,” alisema Dk. Pettis.

Alitoa wito kwa Watanzania kutumia Nyuki Marathon kama jukwaa la kuelimisha jamii, kuwahusisha vijana na kuunga mkono juhudi za Serikali na sekta binafsi katika kulinda na kuendeleza sekta ya nyuki.