27
Jun

Ziwa Duluti Laibua Mwelekeo Mpya wa TFS Kutangaza Vivutio vya Misitu

Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeitaka taasisi hiyo kuandaa siku maalum ya kitaifa kwa ajili ya kutangaza fursa za utalii na uwekezaji katika vivutio vya utalii kwenye Hifadhi za Misitu, huku ikiweka msisitizo kwenye misitu yenye vivutio vya kipekee kama Ziwa Duluti kuwa kitovu cha utalii wa ndani na chanzo cha mapato kwa jamii na serikali.

Kauli hiyo ilitolewa Juni 25, 2025 na Mjumbe wa Bodi hiyo, Mhandisi Enock Emmanuel Nyanda, wakati wa ziara ya siku ya pili ya Bodi ya TFS katika Kanda ya Kaskazini, iliyofanyika kwenye eneo la hifadhi ya Ziwa Duluti, wilayani Arumeru mkoani Arusha.

“Tanzania imejaa vivutio vya kipekee vilivyomo ndani ya Hifadhi za misitu, lakini havijatumiwa kikamilifu. Tuna vivutio kama Ziwa Ngosi lililoko Uporoto, Mbeya – la pili kwa ukubwa barani Afrika kwa maziwa ya asili ya milipuko ya volkano – lakini hakuna mwekezaji hata mmoja. TFS inapaswa kuandaa ‘Siku ya Utalii wa Misitu’ kutangaza hazina hii,” alisema Nyanda, ambaye pia Mkurugenzi Msaidi Idara ya Uratibu wa Sekta Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Kwa mujibu wa Nyanda, uwekezaji uliofanyika Ziwa Duluti kupitia kampuni ya SS Camps unaoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Mwanadada Suzan Minja, unapaswa kuigwa na kuhamasishwa kwenye misitu mingine nchini ili kufungua fursa za kiuchumi, ajira na utalii wa ndani.

Awali, Mhifadhi anayesimamia Hifadhi ya Ziwa Duluti, Peter Myonga, aliwapokea wajumbe wa Bodi na kuwaeleza kuwa eneo la Ziwa Duluti linaendelea kuboreshwa kwa kuimarisha miundombinu ya utalii ikiwemo ujenzi wa vyumba vya malazi, mgahawa na njia za kutembelea maeneo ya mapangoni ambako hufanyika ibada za jadi.

“Vyumba 10 vya kulala wageni viko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Pia tunaendeleza eneo la mgahawa litakalosaidia wageni kupata huduma muhimu wakati wa matembezi,” alisema Myonga.

Mwekezaji katika eneo hilo, Bi. Suzan Minja, alisema uwekezaji unaofanyika unalenga kuongeza ajira kwa vijana wa eneo hilo, kukuza uchumi wa jamii na kusaidia uhifadhi wa mazingira kwa kuzingatia matumizi rafiki ya rasilimali.

“Tulipokuta eneo hili halikuwa na miti, lakini tumejenga kwa kuzingatia mipaka ya hifadhi na kuhifadhi miti yote iliyokuwepo. Hii ni njia endelevu ya kuleta maendeleo pasipo kuharibu mazingira,” alisema Bi. Minja.

Nyanda pia alisisitiza umuhimu wa TFS kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na wadau wa mazingira kuandaa maonesho ya kitaifa yatakayojulikana kama ‘Siku ya Misitu Tanzania’ ili kuonesha bidhaa, huduma na fursa zinazopatikana katika misitu ya asili na mashamba ya miti.

“TFS si taasisi ya kukusanya tu mapato, bali ni mhimili wa uhifadhi, uendelezaji wa mazingira na uchumi wa kijani. Misitu yetu inaweza kuwa mazao ya utalii kama ilivyo kwa wanyamapori,” alieleza.

Ziara hiyo ya Bodi ya Ushauri ya TFS inalenga kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo, usimamizi wa misitu, ukusanyaji wa mapato na ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi katika kanda mbalimbali nchini.