19
Aug

Waziri Mkuu ataka upandaji miti mji wa Serikali kukamilika

Dodoma. Katika kukamilisha azma ya Serikali ya Dodoma ya kijani, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo ya ukamilishwaji wa zoezi la upandaji miti katika Mji wa Serikali Mtumba ili kuufanya mji huo kuwa na hadhi ya makao makuu ya nchi.

 Majaliwa ametoa maagizo hayo Leo Jijini Dodoma katika uzinduzi wa programu ya upandaji miti katika Mji wa Serikali kuelekea kilele cha Siku ya Mazingira duniani itakayofanyika Juni 5, 2022.

Majaliwa amewataka Makatibu wakuu wa Wizara zilizojengwa kwenye mji huo kuifanya programu hiyo kuwa endelevu kwa kushirikiana na wataalamu kuhakikisha miti na nyasi zinazopandwa zinatunzwa kikamilifu.

Pia amewataka Wakala wa huduma za misitu (TFS) na Wakala wa barabara mijini na vijijini (Tarura) kusimamia upandaji miti katika hifadhi za barabara ili kwenda sambamba na mpango huo huku akiwataka wakuu wa wilaya kutoa elimu ya upandaji na utunzaji wa nyasi na miti katika eneo hilo na mipaka yake.

Aidha Majaliwa ametoa siku sita kwa taasisi zinazohusika na ujenzi wa miundombinu ya Mji huo ikiwemo Tanesco , TPDC, Duwasa, TTCL, Temesa , Jeshi la polisi, zimamoto na uokoaji kukamilisha maandalizi yatakayowezesha kuanza kwa ujenzi wa miundombinu ya huduma hizo na kutoa mrejesho wa mradi huo.

“Taasisi zote zinazohusika na ujenzi wa miundombinu katika mji huu zikamilishe haraka sana taratibu za maandalizi yote yatakayowezesha ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya huduma hizo na Ofisi yangu ipate mrejesho wa hatua za maandalizi ifikapo Juni 6 mwaka

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk John Jingu amesema katika zoezi hilo la upandaji miti kwa awamu ya kwanza miti 550,000 ya aina mbalimbali itapandwa kwenye mji wa Serikali hususan kwenye maeneo ya Wizara, barabara na mipaka ya mji pamoja kuweka mifumo ya miundombinu ya umwagiliaji itakayosimamiwa na Tume ya Taifa ya umwagiliaji (NIRC).

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) Dos Santos Silayo amesema mwaka 2017 Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais alizindua Kampeni ya upandaji miti ya Dodoma ya kijani na tangu hapo TFS imesimamia zoezi hilo ambapo kwa kipindi cha miaka minne Dodoma imepandwa miti 575,000 huku miti 26,200 ikipandwa mji wa Serikali chini ya oparesheni ya Mkurugenzi wa Jiji.

“Sambamba na upandaji huo wa miti Ofisi yako itaingia mikataba ya makubaliano na taasisi zinazotekeleza programu hii kwa lengo la kuhakikisha kuwa miti itakayopandwa inatunzwa na kutekeleza dhana ya Mji wa Serikali