05
Dec

Wazazi Wasisitizwa Kukuza Uelewa wa Uhifadhi wa Misitu Kwa Watoto Wao

Jamii inayoishi karibu na maeneo ya hifadhi imetakiwa kuhakikisha watoto wanashirikishwa kikamilifu katika uhifadhi wa misitu na kulelewa katika msingi imara wa maadili, ili kujenga kizazi chenye uelewa na mtazamo chanya kuhusu kulinda rasilimali za taifa.

Wito huo umetolewa leo Disemba 4,2025 na Mhifadhi Mwaandamizi wa Shamba la Miti Wino, Glory Kasmir, wakati wa mahafali ya Watoto wa Awali na Darasa la Saba katika Shule ya St. Monica Pre and Primary School, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, mkoani Ruvuma.

Akizungumza kwenye mahafali hayo, Kasmir alisema malezi bora na elimu ya mapema kuhusu umuhimu wa misitu ni msingi muhimu wa kulijenga taifa lenye wananchi wanaotambua nafasi yao katika kulinda mazingira na vyanzo vya rasilimali.

Alisema pamoja na jitihada za Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), bado kumekuwepo na ongezeko la vitendo vinavyohatarisha ustawi wa watoto na kuathiri misitu, hivyo kuhitaji hatua za pamoja kutoka kwa wadau wote.

“Ni muhimu jamii kuhakikisha watoto wanakua wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu thamani ya misitu. Hii itasaidia si tu kulinda rasilimali zetu, bali pia kujenga tabia chanya zinazohakikisha ustawi wa mazingira na vizazi vijavyo,” alisema Kasmir.

Aidha, alisisitiza kuwa jamii inayozunguka hifadhi ina wajibu wa kwanza kuhakikisha misitu inasimamiwa ipasavyo, kwa kuwa athari za uharibifu wa mazingira huathiri moja kwa moja maisha yao, ikiwamo upatikanaji wa maji, hewa safi na uthabiti wa ikolojia.

Kasmir alibainisha kuwa jukumu la uhifadhi haliwezi kuachwa kwa TFS pekee, hivyo kuhitaji ushiriki wa pamoja wa wazazi, walimu, viongozi wa jamii na watoto, ili kuhakikisha misitu inabaki salama kwa manufaa ya taifa.