07
Feb
WAHIFADHI WA JESHI LA UHIFADHI TFS WAPANDISHWA VYEO
JESHI la Uhifadhi la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) limewapandisha vyeo askari 60 na maafisa 30 wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, katika hatua inayolenga kuimarisha nidhamu, kuongeza morali kazini na kulinda rasilimali za misitu na nyuki kwa ufanisi zaidi.
Uvishwaji wa vyeo hivyo umefanyika leo katika ukumbi wa Social uliopo Shamba la Miti Sao Hill, mkoani Iringa, na kuhudhuriwa na viongozi wa TFS, askari wa jeshi hilo pamoja na wadau wa uhifadhi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamanda wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Getrude Nganyagwa, aliyemwakilisha Kamishna wa Jeshi la Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema kupandishwa vyeo kwa askari hao ni matokeo ya nidhamu, uzalendo, bidii na kujituma katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi.
Alisisitiza kuwa vyeo hivyo si heshima pekee, bali ni dhamana mpya inayohitaji uwajibikaji mkubwa, uadilifu na utii wa sheria, ili kulinda rasilimali za taifa kwa masilahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Vyeo mlivyopata leo ni matokeo ya juhudi zenu binafsi. Ni wajibu wenu kuvilinda kwa nidhamu, uadilifu na bidii kazini. Zingatieni sheria na kanuni za Jeshi la Uhifadhi pamoja na misingi ya utumishi wa umma, ili rasilimali za misitu na nyuki zilindwe ipasavyo kwa manufaa ya taifa,” alisema Nganyagwa.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia TFS inaendelea kuimarisha Jeshi la Uhifadhi kwa kulipa kipaumbele suala la motisha kwa watumishi wake, sambamba na kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya uharibifu wa misitu, uvamizi wa hifadhi na uhalifu wa rasilimali za asili.
Kwa upande wao, baadhi ya askari na maafisa waliovishwa vyeo walieleza kuwa hatua hiyo imeongeza ari na moyo wa kujituma kazini, wakiahidi kuendeleza nidhamu, kusimamia sheria za uhifadhi kwa haki, na kushirikiana kwa karibu na jamii zinazozunguka hifadhi katika kulinda misitu na nyuki.
Walisema kuwa ushirikiano kati ya Jeshi la Uhifadhi na wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya uhifadhi endelevu na kupunguza migogoro inayohusiana na matumizi ya rasilimali za misitu.