24
Sep

VIONGOZI MUFINDI WAKUMBUSHWA KUIMARISHA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA MOTO WA MISITU

Na Mwandishi wetu - Iringa

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Sao Hill kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, wamewakutanisha wadau mbalimbali Wilayani Mufindi tarehe 24 Septemba,2026 katika kikao maalum cha kukumbushana na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na matukio ya moto wa misitu, hususan katika kipindi cha kiangazi.

Kikao hicho kimejikita katika kuwakumbusha viongozi kuhusu wajibu wao wa kusimamia matumizi sahihi ya moto katika maeneo yao, pamoja na kuhakikisha mikakati iliyowekwa awali ya kuzuia na kudhibiti moto inatekelezwa ipasavyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa amewataka viongozi wa ngazi zote kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuzuia moto, akisisitiza kuwa ulinzi wa misitu unahitaji ushirikiano wa viongozi, taasisi na wananchi kwa ujumla.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha mikakati tuliyojiwekea inasimamiwa na kutekelezwa katika maeneo yetu. Viongozi tusisubiri moto utokee ndipo tuchukue hatua, bali tuweke nguvu katika kuzuia ,” Amesema Dkt. Salekwa

Amesisitiza kuwa viongozi wanatakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na uanzishaji wa moto na kuhakikisha suala la utoaji wa vibali vya uanzishaji wa moto linasimamiwa vizuri ili kuondokana na matukio ya moto.

Hata hivyo ametoa wito kwa watu wote wenye mashamba ya miti makubwa na madogo kuhakikisha mashamba hayo yanafanyiwa usafi na kuwekwa barabara kinga moto ili kupunguza athari za matukio ya moto katika mashamba ya miti na misitu ya asili.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi Reuben Chongolo akimkaribisha Mgeni rasmi, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa maeneo kuhakikisha wananchi wanafahamu taratibu za matumizi sahihi ya moto, hasa wakati wa kufanya shughuli za kilimo, ufugaji na shughuli nyingine zinazohitaji matumizi ya moto.

Naye Diwani wa Kata ya Mdabulo Mhe. Marco Shayo aliyeshiriki kikao hicho ameeleza kuwa viongozi wa ngazi za kata na vijiji wana nafasi kubwa katika kuzuia moto wa misitu kwa kuwa wako karibu na wananchi na kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi huku wakihakikisha sheria na kanuni za usimamizi wa uanzishaji wa moto zinasimamiwa ipasavyo.

“Tumepewa wajibu wa kuwasimamia wananchi na kuhakikisha elimu tunayopata hapa inawafikia na ndio maana kijiji chetu cha Kidete kimekua cha mfano na kinara wilayani Mufindi kwani tumehakikisha sheria zote za uanzishaji moto zinafutwa ili kuondokana na matukio ya moto". Amesema Mhe. Shayo

Naye Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba upande wa Uendelezaji Msitu PCO Said Singano amesema moto wa misitu unaweza kusababisha hasara kubwa kwa rasilimali za misitu, mazingira na shughuli za kiuchumi zinazotegemea misitu, hivyo viongozi wanapaswa kuimarisha usimamizi katika maeneo yao.

Aidha, kikao hicho kimehimiza ushirikiano wa karibu kati ya TFS, viongozi wa serikali za mitaa, watendaji na wananchi katika kutoa taarifa za mapema kuhusu viashiria vya moto na kuchukua hatua za haraka pale tukio linapotokea.

TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill imeendelea kutoa elimu kwa jamii zinazozunguka shamba hilo kuhusu matumizi sahihi ya moto, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda misitu na kuhakikisha rasilimali hiyo inaendelea kuwa na manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.