18
Feb
UBUNIFU,TEHAMA NA NIDHAMU VYABEBA MAFANIIO YA TFS
Morogoro, Tanzania
Serikali imeipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano, huku ikiutaka wakala huo kuongeza kasi ya ulinzi wa rasilimali za misitu, ubunifu wa vyanzo vya mapato na maendeleo ya utalii wa ikolojia ili kuchangia azma ya taifa ya kufikisha watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Maelekezo hayo yametolewa leo Februari 18, 2026 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, wakati akifungua Mkutano wa Nne wa Viongozi na Makamanda wa TFS wa mwaka 2025/2026 kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, uliofanyika mkoani Morogoro.
Akizungumza katika mkutano huo, Chande alieleza kuwa TFS imeonyesha uwezo mkubwa katika usimamizi wa misitu, lakini sasa inapaswa kuimarisha zaidi vituo vya ulinzi katika maeneo yenye changamoto ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la utegemezi wa jamii kwa rasilimali za misitu.
Katika tathmini ya sekta, imeelezwa kuwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za misitu imefikia takribani 350,000 kwa mwaka, huku mapato yakivuka Sh2.9 bilioni, mafanikio yanayoonyesha kuimarika kwa utalii wa ikolojia nchini.
Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, amesema TFS imewekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya TEHAMA kupitia mfumo wa eMisitu wenye moduli 11, unaosaidia ufuatiliaji wa mazao ya nyuki, usimamizi wa mashamba ya miti, uuzaji mtandaoni na huduma za utalii. Mfumo huo umeongeza uwazi, ufanisi na ukusanyaji wa maduhuli.
Katika kipindi cha Mpango Mkakati wa Tatu (2020/21–2025/26), TFS imeajiri watumishi 588 na kufikisha jumla ya 2,466, wakiwamo askari wa Jeshi la Uhifadhi 1,669. Aidha, migogoro 423 kati ya 438 (96%) imetatuliwa, na hekta 612,300.9 kutolewa kwa wananchi katika vijiji 112 kufuatia maelekezo ya mamlaka husika.
Katika eneo la biashara ya mazao ya misitu, zaidi ya mita za ujazo milioni 4.4 zilivunwa huku mauzo ya nje yakiongezeka kwa asilimia 130 ndani ya miaka mitano. Sekta ya nyuki imeendelea kung’ara kwa uzalishaji wa wastani wa tani 33,861, na tani 9.5 za asali kuuzwa nje zenye thamani ya Sh93.3 bilioni, huku asilimia 96 ya sampuli zikikidhi viwango vya soko la Ulaya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Chiku Abdallah Gallawa, amesema bodi itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuimarisha ubunifu wa vyanzo vipya vya fedha, ikiwamo mkakati wa malipo ya huduma za kiikolojia, huku akisisitiza nidhamu, weledi na utu katika utendaji.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abasi, aliyewakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bernard Patrice Marcelline, amesisitiza umuhimu wa kuoanisha mipango ya TFS na Ilani ya Uchaguzi 2025–2030 pamoja na ahadi za bajeti ya 2025/26, huku maandalizi ya Mpango Mkakati wa Nne (2026/27–2030/31). Mkutano huo wa wiki moja, unaojumuisha pia mafunzo ya uongozi wa kimkakati, afya ya akili na bonanza la michezo kwa ajili ya kujenga mshikamano, unatajwa kuwa jukwaa muhimu la kupima utekelezaji wa malengo na kuweka mwelekeo mpya wa sekta.