07
Oct

UBORA WA MAZAO YA NYUKI WAMVUTIA MBUNGE BHUTAN

Na Mwandishi Wetu, Arusha

ARUSHA: Mbunge wa Bunge la Bhutan, Tashi Tenzin, amepongeza ubora wa mazao ya nyuki yanayoonyeshwa katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU 153), unaofanyika Arusha.

Tenzin amesema amevutiwa na ubora wa bidhaa hizo, akisema ni nadra kukutana na asali yenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa bila kuongezewa vitu vingine.

Amesema hali hiyo inaonyesha kuwa uzalishaji na uvunaji wa mazao ya nyuki nchini unazingatia utaalamu, matumizi ya vifaa bora na teknolojia za kisasa.

“Hongereni sana kwa bidhaa bora. Si kawaida kukuta asali ambayo haijaongezewa kitu chochote. Hii ni hatua nzuri na inaonyesha Tanzania inazingatia viwango katika bidhaa zake,” amesema.

Mbunge huyo pia ameipongeza Tanzania kwa uzalishaji wa asali, akirejea takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) za mwaka 2024 zinazoitaja Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa asali barani Afrika.

Amesema angependa kupata uzoefu kuhusu mbinu zinazotumika nchini katika uzalishaji wa mazao ya nyuki yenye ubora.

“Bidhaa zenu zina ubora wa kimataifa. Nataka pia kujifunza mbinu mlizotumia kufikia kiwango hiki. Nitarudi katika banda lenu kupata uzoefu zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Mhifadhi Subira Matimbwa, Afisa Nyuki Msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), amesema ubora wa mazao ya nyuki unatokana kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa mazingira na misitu asilia, pamoja na matumizi ya vifaa bora wakati wa uvunaji.

“Tunashukuru kwa pongezi. Bidhaa zetu zinatokana na mazingira asilia tuliyonayo, pamoja na matumizi ya vifaa vya kisasa na utaalamu wakati wa uvunaji,” amesema.

Mkutano wa IPU 153 unaendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ambapo Tanzania inashiriki katika kuonyesha fursa mbalimbali za uhifadhi, utalii na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na nyuki