04
Oct

TFS YAWEKA MKAKATI KUKOMESHA BIASHARA HARAMU ZA MAZAO YA MISITU

Na Mwandishi Wetu – Iringa

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, umeweka mikakati ya kuimarisha doria na udhibiti wa vituo vya ukaguzi ili kukomesha uharibifu wa misitu, uvunaji, usafirishaji na biashara haramu ya mazao ya misitu na nyuki.

Mikakati hiyo imewekwa katika kikao cha siku nne cha Menejimenti ya Kanda kilichofanyika Manispaa ya Iringa kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 1, 2026, kikilenga kutathmini utendaji, mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya Kanda.

Akifungua kikao hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi (SACC) Getruda Nganyagwa, ambaye ni Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, aliwataka wahifadhi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia utu.

Nganyagwa aliwataka wahifadhi kuimarisha ushirikiano na jamii zinazozunguka misitu ya hifadhi ili wananchi washiriki kikamilifu katika usimamizi na ulinzi wa rasilimali za misitu na nyuki.

Pia alielekeza vituo vya ukaguzi wa mazao ya misitu na nyuki kusimamiwa ipasavyo ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na kuhakikisha sheria na taratibu za uvunaji, usafirishaji na biashara ya mazao hayo zinafuatwa.

“Ni muhimu kuimarisha doria za kimkakati ili kuziba mianya ya uvunaji haramu, usafirishaji na utoroshaji wa mazao ya misitu na nyuki, pamoja na kukomesha biashara holela ya mazao hayo,” alisema.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wahifadhi 45 kutoka wilaya 19, Hifadhi za Mazingira Asilia tatu, Shamba la Nyuki pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Kanda.

Katika kikao hicho, wajumbe walijadili masuala mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu na kupitisha maazimio yanayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki, uwajibikaji, ushirikiano na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Maazimio hayo pia yamelenga kuhakikisha mipango na malengo ya Kanda yanafikiwa kwa ufanisi, huku usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki ukipewa kipaumbele.