05
Jun

TFS YATUNUKIWA NA TUZO YA KAMPENI BORA YA UPANDAJI MITI NCHINI

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetunukiwa Tuzo ya Kampeni Bora ya Upandaji Miti kwa mwaka 2025, kutokana na mchango wake mkubwa katika kuhamasisha wananchi na taasisi mbalimbali kushiriki upandaji miti, kusambaza miche na kuelimisha umma kuhusu utunzaji wa mazingira.

Tuzo hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika leo, Juni 5, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alisema ushindi huo ni uthibitisho wa juhudi za TFS kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini katika kutekeleza kampeni ya kitaifa ya kupanda miti.

“Tuzo hii imetambua mchango wa TFS katika kusambaza miche, kupanda miti na kutoa elimu ya mazingira. Tunaiona kama motisha mpya ya kuhakikisha elimu kuhusu aina bora za miti, maeneo yanayofaa kwa upandaji na mbinu za kuitunza inawafikia Watanzania wengi zaidi,” alisema Prof. Silayo.

Alieleza kuwa TFS imekuwa mstari wa mbele kutumia teknolojia za kisasa kama satelaiti na ndege zisizo na rubani (drones) kwa ajili ya doria na ufuatiliaji wa misitu, hatua iliyosaidia kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za ulinzi wa mazingira.

“Tunatumia mifumo ya kisasa ya doria ya kimkakati ambayo hutoa matokeo ya moja kwa moja. Teknolojia hizi – zikiwemo drones na satelaiti – zimetuwezesha kulinda misitu kwa weledi na kwa gharama nafuu,” alibainisha.

Prof. Silayo aliongeza kuwa mafanikio ya TFS yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wa karibu kati ya wakala huo, taasisi za serikali, wananchi na mabalozi wa mazingira wanaolelewa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

“Kuanzia uzalishaji wa mbegu hadi kupanda miti, tunashirikiana na wadau wote ili kuhakikisha elimu ya mazingira inawafikia Watanzania wote na kampeni za upandaji miti zinakuwa endelevu,” alisema.

Licha ya changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, Prof. Silayo alisema Tanzania bado inaendelea kushikilia nafasi ya pili barani Afrika kwa kuwa na urithi mkubwa wa bioanuai, ikitanguliwa na Brazil pekee.

“Ni kweli tuna changamoto, lakini hatua madhubuti zilizochukuliwa na serikali – hasa kwenye uwekezaji wa nishati mbadala – zinaonyesha mwelekeo mzuri. Serikali imewekeza kwenye nishati safi ya kupikia hivyo kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa,” alieleza.

Kamishna huyo alitoa wito kwa Watanzania wote, taasisi na mashirika kushiriki kikamilifu katika juhudi za kitaifa za kupanda miti, kulinda misitu na kubadili tabia zinazochangia uharibifu wa mazingira.

“Kila mmoja ana jukumu la kulinda mazingira. Tunashukuru vyombo vya habari kwa mchango wao wa kutoa elimu kwa umma na tunawaomba waendelee kufanya hivyo. Tukishirikiana, tutajenga Tanzania yenye mazingira bora kwa sasa na kwa vizazi vijavyo,” alihitimisha.

Katika hotuba yake ya kufunga maadhimisho hayo, Makamu wa Rais, Dkt. Mpango, aliwataka Watanzania kuwajibika sasa kulinda mazingira kwa kupunguza utupaji hovyo wa taka, kulinda vyanzo vya maji, na kuhamia nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti.

Alisisitiza kuwa uchafuzi wa mazingira, utegemezi wa kuni na mkaa na matumizi ya plastiki visivyo na tija ni chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa bioanuai nchini.

“Serikali tayari imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, na imeanza kutekeleza agizo la kuhamisha taasisi zinazolisha watu 100 au zaidi kwa siku kwenda kutumia nishati safi. Taarifa zinaonyesha taasisi 762 zimehamia kutumia gesi asilia, umeme au biogas. Hili ni jambo la kutia moyo,” alisema.

Dkt. Mpango aliwatunuku tuzo washindi mbalimbali wa mazingira na kutoa pongezi kwa wadau, wajasiriamali na vyombo vya habari kwa kuendeleza kampeni za upandaji miti na kupunguza taka za plastiki.

“Tukishirikiana, tutaacha urithi wa mazingira bora kwa vizazi vijavyo,” alisisitiza.