02
Oct
TFS YASHIRIKI USAFI, UPANDAJI MITI WORLD CLEANUP DAY KONDOA
Na Mwandishi Wetu – Kondoa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeungana na wananchi, wanafunzi na wadau wa mazingira katika zoezi la usafi na upandaji miti lililofanyika katika Shule ya Sekondari Bicha, Wilaya ya Kondoa, Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya World Cleanup Day 2026.
Zoezi hilo lililofanyika Oktoba 2, 2026, lilihusisha usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya shule na upandaji wa miti 500 ya aina za mizambarau (Syzygium cumini), mti maji (Trichilia emetica) na mpera (Psidium guajava).
TFS kupitia Ofisi ya Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kondoa ilishiriki zoezi hilo kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la GO PLANT TANZANIA pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bicha.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Nhamanilo Kwagilwa, aliwataka wananchi kuendelea kushiriki katika uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kulinda vyanzo vya maji na kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino.
Kwagilwa pia alizitaka halmashauri zote nchini kuwa na vitalu vya miche ya miti ili kuongeza upatikanaji wa miche na kuchangia katika kufikia malengo ya kitaifa ya upandaji miti.
Katika maadhimisho hayo, wanafunzi walipewa elimu kuhusu utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa lengo la kuwajengea uelewa na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za uhifadhi katika jamii.
Kwa upande wake, Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kondoa, CO I Fred Steven James, alitoa shukrani kwa Serikali, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), viongozi, GO PLANT TANZANIA, uongozi wa Shule ya Sekondari Bicha, wanafunzi, wananchi na wadau wengine kwa kushiriki katika kufanikisha maadhimisho hayo.
James alisema ushirikiano huo ni muhimu kuendelezwa ili kuongeza uhamasishaji wa jamii kushiriki katika usafi wa mazingira, upandaji miti na uhifadhi wa rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Naibu Waziri aliipongeza TFS kwa mchango wake katika uhifadhi wa misitu na mazingira, ikiwemo upandaji na ugawaji wa miche ya miti kwa jamii.
Katika kutambua mchango huo, TFS ilikabidhiwa Cheti cha Shukrani kwa kushiriki katika World Cleanup Day 2026 na kampeni ya “Dodoma Tunajitokeza”, inayolenga kuhamasisha jamii kushiriki katika usafi, upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), vyombo vya habari na wadau wengine wa mazingira.