
21
Nov
TFS yapiga jeki sekondari Itala, kituo cha polisi Igoma
Mbeya. Shule ya Sekondari ya Itala iliyoko Kata ya Igoma, Wilaya ya Mbeya Vijini imepokea msaada wa madawati 120 kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Shamba la Miti Kiwira.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Kiwira, Thadeus Shirima amesema pamoja na kutoa madawati hayo na mifuko 180 kwaajili ya kituo cha Polisi cha Igoma wataongeza Sh5 milioni ili kurahisisha ujenzi wa kituo cha polisi.
"Pamoja na kuchangia shughuli za maendeleo lakini tumekuwa tukitoa ajira za muda kwa wananchi wa vijiji vya hapa ambapo kila mwaka zaidi ya wananchi 300 hunufaika katika upodoaji wa matawi ya miti, doria, kupanda miti na kupalilia.
Mashamba ya misiti ni miongoni mwa misitu ya hifadhi za serikali kuu zinazosimamiwa na TFS ambayo idadi yake ni 24 ikiwemo Kiwira.
"TFS imeweka mikakati ya kuendeleza na kuanzisha mashamba ya miti ili kuongeza mapato ya serikali na kutoa ajira kwa wananchi wanaotuzunguka.
Shirima amesema kwa kipindi cha miaka minne TFS kupitia Shamba la Miti Kiwira imechangia miradi ya maendeleo kwa vijiji vinavyowazunguka kufikia thamani ya Sh42 milioni.
Hata hivyo Shirima ameongeza kwa sasa shamba hilo halina eneo la wazi na changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni uchomwaji wa moto, uvamizi wa watu ndani ya maeneo ya Shamba kwaajili ya kuendesha shughuli za kilimo na malisho ya mifugo na kusababisha miti iliyopangwa kuharibiwa na hatimaye kufa.
"Kukabiliana na changamoto hizi tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi juu ya madhara yake na mwitikio umekuwa mzuri kwani baadhi ya wananchi wamekuwa wakitoa taarifa za moto na matukio mengine ya uvamizi," alisema Shirima.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua akipokea madawati na saruji hizo amesema ni vyema wananchi wakaendelea kulinda maeneo hayo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
"Tunaimani kubwa na nyie katika uhifadhi na kulinda rasilimali na kujihusisha katika shuguli za maendeleo kwa jamii katika eneo hili.
"Tumejifunza kupitia kwenu kwa moyo mnaoufanya sababu sio lazima kwa hiki mnachokifanya bali ni moyo wa mtu lakini mmekuwa wakarimu na kuona mnaowajibu wa kufanya hili," amesema Chuachua.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Itala, Erneo Mwakingili amesema hitaji lao lilikuwa madawati 100 lakini kupata 20 zaidi itasaidia sababu Januari inakuwa na ongezeko la wanafunza wanaojiunga kidato cha kwanza n hivi sasa wapo katika mchakato wa ujenzi wa mabweni.