23
Sep

TFS YAKABIDHI MADAWATI 50 SHULE YA MAZINYUNGU

KILOSA. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Mashariki, umekabidhi madawati 50 yenye thamani ya Sh milioni 12 kwa Shule ya Msingi Mazinyungu wilayani Kilosa, Morogoro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kurejesha kwa jamii inayoshiriki katika uhifadhi wa misitu.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo, Jumatano Septemba 23, 2026, ambapo kwa niaba ya Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, SACC Mathew Ntilicha, Mhifadhi Misitu Mwandamizi, Dotto Ndumbikwa amesema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa taasisi hiyo kushirikiana na jamii na kurejesha sehemu ya manufaa kwa wananchi wanaoshiriki katika kulinda rasilimali za misitu.

Ndumbikwa amesema TFS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kulinda na kuhifadhi misitu, akisisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali hiyo inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Jamii ina nafasi kubwa katika kuhakikisha misitu inalindwa na kutunzwa. TFS itaendelea kushirikiana na jamii na wadau wengine katika kuhakikisha rasilimali za misitu zinahifadhiwa,” amesema Ndumbikwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, ameishukuru TFS kwa msaada huo akisema umefika wakati muafaka kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo.

Shaka amesema Serikali haiwezi kutekeleza kila jukumu bila ushirikiano wa wadau, hivyo ameitaka TFS kuendelea kuunga mkono shule nyingine zenye mahitaji katika maeneo yake.

Amesisitiza pia umuhimu wa jamii kupanda na kutunza miti, akisema Kilosa haipaswi kuwa jangwa, huku akiwataka walimu kutumia nafasi yao kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ili ujumbe huo uwafikie wazazi na jamii kwa ujumla.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazinyungu, Kajika Gallani, amesema msaada huo umepunguza changamoto ya upungufu wa madawati na kuwawezesha wanafunzi 150 waliokuwa wakisomea bila kuwa na sehemu za kukaa kupata madawati.

Hata hivyo, amesema shule hiyo bado ina upungufu wa madawati 50, akiwataka wadau wengine kuiga mfano wa TFS kwa kusaidia kukamilisha mahitaji yaliyosalia