22
Sep
TFS YAIMARISHA UPATIKANAJI WA MBEGU BORA ZA MITI
Mwandishi Wetu – Iringa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wahifadhi wa misitu katika ukusanyaji wa mbegu bora za miti, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mbegu zenye ubora kwa ajili ya uzalishaji wa miche na upandaji miti nchini.
Mafunzo hayo yameanza leo Septemba 22, 2026 katika Shamba la Miti Sao Hill, mkoani Iringa, yakifunguliwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Kurugenzi ya Huduma Saidizi na Utawala TFS, DCC Emmanuel Wilfred Kiboko, aliyesisitiza umuhimu wa kutumia utaalamu na mbinu za kisayansi katika ukusanyaji wa mbegu.
DCC Kiboko amesema upatikanaji wa mbegu bora ni msingi wa kuzalisha miche yenye ubora na hatimaye kuimarisha misitu yenye afya na tija, huku akieleza kuwa TFS itaendelea kuwekeza katika mafunzo ya watumishi ili kuendana na teknolojia za kisasa na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
“Ujuzi huu mnaoendelea kuupata tuutumie tunapoenda kutekeleza majukumu, kwani malengo ya taasisi ni kuhakikisha tunakuwa na misitu endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema DCC Kiboko.
Amewataka wahifadhi hao kuzingatia miongozo, taratibu na kanuni za utumishi wa umma, kutumia ujuzi wanaoupata katika maeneo yao ya kazi na kutunza vifaa watakavyokabidhiwa ili viweze kutumika kwa muda mrefu.
Akitoa taarifa kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja wa Sehemu ya Baiolojia ya Mbegu za Miti, SACC Fandey H. Mashimba, amesema kada ya wavunaji mbegu imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa watumishi kutokana na kustaafu, hali iliyosababisha TFS kubaki na watumishi watano ambao nao wanakaribia kustaafu.
Mashimba amesema kupitia mradi wa “Enhanced Conservation of 57 Highly Threatened Tanzanian Tree Species”, unaofadhiliwa na Franklinia Foundation, kuratibiwa na Missouri Botanical Garden ya Marekani na kutekelezwa na TFS, seti 10 za vifaa maalumu vya kukwea na kuvunia mbegu zimenunuliwa pamoja na kugharamia mafunzo kwa watumishi wapya 10.
“Mafunzo haya yataimarisha utambuzi, uchaguzi na ukusanyaji wa mbegu kutoka kwenye miti bora kwa kufuata kanuni za kitaalamu, kuongeza wataalamu nchini na kusaidia kukidhi mahitaji ya mbegu bora za miti,” amesema Mashimba.