03
Nov
TFS YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA, WATUMISHI 148 WAPATIWA ELIMU
DODOMA | 03 Novemba 2026
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), CC Prof. Dos Santos Silayo, amewataka maafisa na askari wa Wakala huo kuwa mabalozi wa kuzuia na kupambana na rushwa, kuzingatia uongozi bora na kusimamia maadili katika maeneo yao ya kazi.
Wito huo umetolewa Novemba 3, 2026, wakati akifunga semina elekezi ya siku mbili kuhusu maadili, uongozi bora na mapambano dhidi ya rushwa, iliyofanyika jijini Dodoma na kuwashirikisha jumla ya maafisa 148 kutoka Makao Makuu ya TFS na Kanda ya Kati.
Prof. Silayo amewataka washiriki kutumia maarifa waliyoyapata kuleta mabadiliko katika taasisi kwa kujiepusha na vitendo vinavyokiuka maadili ya utumishi wa umma, ikiwemo rushwa, ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka na kutokuwa waadilifu.
“Najua semina hii itawapa uwezo wa kuwa mabalozi wa kuzuia rushwa. Kupitia mada zilizowasilishwa, nimefahamu kuwa mmepata uelewa kuhusu madhara ya rushwa na kukosa maadili kwa mtumishi wa umma. Hivyo, tushirikiane na kusaidiana katika utekelezaji wa majukumu yetu, kila mmoja awe msaada kwa mwenzake,” amesema Prof. Silayo.
Awali, Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Kurugenzi ya Huduma Saidizi na Utawala, DCC Emmanuel Wilfred Kiboko, amesema semina hiyo imejikita katika mada kuu zikiwemo Mkakati wa TFS wa Kukabiliana na Rushwa wa mwaka 2023/2024 hadi 2029/2030, hali ya maadili na mashauri ya kinidhamu kwa watumishi wa TFS, pamoja na namna ya kuzuia na kupambana na rushwa mahali pa kazi kwa kuzingatia uzoefu katika sekta ya misitu.
Amesema washiriki pia wamepatiwa elimu kuhusu vitendo vya rushwa vinavyoweza kufanywa na watumishi, madhara yake na hatua zinazopaswa kuchukuliwa, huku mwezeshaji Otenyo Ollech Maichael kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) akitoa elimu kuhusu masuala ya rushwa. Semina hiyo pia ilitoa fursa ya majadiliano na kubadilishana uzoefu kuhusu njia bora za kuzuia vitendo hivyo katika maeneo ya kazi.
Kwa upande wao, washiriki wameishukuru TFS kwa kuandaa semina hiyo na kupendekeza mafunzo ya aina hiyo yaendelee kutolewa katika majukwaa mbalimbali ya Wakala, kuanzia ngazi ya Makao Makuu hadi vituo na maeneo mengine ya utendaji.
Semina hiyo ilianza Novemba 2 na kufungwa rasmi Novemba 3, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za TFS kuimarisha uadilifu, uwajibikaji na mifumo ya kuzuia na kupambana na rushwa katika utekelezaji wa majukumu yake.