18
Oct
TFS YAELIMISHA WANANCHI FURSA NA BIASHARA YA MAZAO YA MISITU
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Sao Hill na TFS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini unaendelea kushiriki katika Mufindi Investment Forum & Expo 2026, inayofanyika katika Viwanja vya Wambi, Mafinga, Wilaya ya Mufindi, kwa kutoa elimu kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya misitu pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.
Kupitia banda la TFS, wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali wanapata fursa ya kujifunza kuhusu mazao ya misitu na namna yanavyoweza kutumika kama chanzo cha ajira, kipato na uwekezaji, ikiwemo uzalishaji na biashara ya magogo, mbao na mazao mengine ya misitu.
TFS pia inaendelea kutoa elimu kuhusu taratibu na masharti ya kufanya biashara ya mazao ya misitu, ikiwemo hatua zinazopaswa kufuatwa na wafanyabiashara ili kuhakikisha biashara hiyo inafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Mbali na elimu, huduma za utoaji wa vibali kwa ajili ya biashara ya mazao ya misitu na usafirishaji wa mazao hayo zinapatikana katika viwanja vya Wambi, hivyo kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kupata huduma hizo kwa urahisi wakati wa maonesho.
Ushiriki wa TFS katika maonesho haya unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu, huku wakinufaika kiuchumi bila kuathiri uendelevu wa misitu na mazingira kwa ujumla.
Sekta ya misitu ina nafasi kubwa katika kuchochea uchumi kupitia uzalishaji wa mazao mbalimbali, ajira, biashara na uwekezaji, sambamba na mchango wake katika uhifadhi wa bioanuai, vyanzo vya maji na mazingira.
TFS inawakaribisha wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali kutembelea banda la TFS katika Mufindi Investment Forum & Expo 2026 ili kupata elimu zaidi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya misitu, taratibu za biashara ya mazao ya misitu pamoja na huduma za vibali vya biashara na usafirishaji zinazotolewa katika viwanja vya Wambi.