07
Oct

TFS SAO HILL YAONGEZEWA NGUVU KAZI

Na Mwandishi Wetu, Iringa

IRINGA: Shamba la Miti Sao Hill limepokea watumishi wapya 18 katika kada mbalimbali, hatua inayolenga kuimarisha nguvu kazi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu katika maeneo mbalimbali ya shamba hilo.

Akizungumza wakati wa kuwapokea watumishi hao, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, aliwataka kuwa na nidhamu, mshikamano na utayari wa kufanya kazi katika mazingira mbalimbali, huku wakitumia uzoefu wa watumishi waliowakuta kujenga uwezo wao.

Yoramu alisema watumishi hao wana wajibu wa kulinda na kujenga taswira nzuri ya taasisi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Kila mmoja wenu anapaswa kuwa tayari kujifunza na kufanya kazi katika mazingira yoyote. Tunataka kuijenga na kuitangaza taasisi yetu kwa mambo chanya, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kulinda taswira ya taasisi ili kufikia malengo iliyojiwekea na ya Serikali kwa ujumla,” alisema Yoramu.

Alisisitiza pia umuhimu wa kushirikiana na watumishi waliowakuta katika maeneo yao ya kazi pamoja na jamii inayozunguka shamba, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

Aidha, aliwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma pamoja na kanuni za Jeshi la Uhifadhi, akisisitiza kuwa nidhamu inapaswa kuwa sehemu ya maisha yao katika kipindi chote cha utumishi.

“Nidhamu isiwe ya muda, bali iwe sehemu ya maisha yenu yote katika utumishi wa umma. Zingatia sheria, kanuni na taratibu, shirikiana na wenzako na tumieni fursa hii kujenga maisha yenu ya sasa na ya baadaye,” alisema.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba anayesimamia Masoko na Matumizi, SCO Peter Nyahende, aliwapatia watumishi hao utangulizi kuhusu Shamba la Miti Sao Hill, ukiwamo muundo wa shamba, shughuli zinazotekelezwa pamoja na namna ya kushirikiana katika majukumu yao.

Nyahende aliwataka pia kujenga mawasiliano mazuri kazini, akisema mawasiliano na ushirikiano ni msingi wa kutengeneza mazingira bora ya kazi na kutatua changamoto zinazojitokeza.

“Ni muhimu kuelewa kwanza mazingira mnayokwenda kufanyia kazi, kujenga mawasiliano mazuri na wenzenu na kujua namna sahihi ya kuwasilisha changamoto pale zinapojitokeza, iwe ni za kikazi au binafsi,” alisema.

Kupokelewa kwa watumishi hao wapya kunatarajiwa kuongeza uwezo wa Shamba la Miti Sao Hill katika utekelezaji wa majukumu yake ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za misitu.