22
Oct
TFS KUIMARISHA UDHIBITI WA MALIASILI ZINAZOSAFIRISHWA KWA MAKONTENA
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unatarajia kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa maliasili kufuatia mafunzo ya kikanda yaliyolenga kukabiliana na biashara haramu ya maliasili kupitia usafirishaji wa mizigo kwa makontena.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya warsha ya kikanda iliyofanyika Libreville, Gabon, Oktoba 20–21, 2026, ambapo washiriki walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Magharibi katika kubadilishana taarifa na kudhibiti biashara haramu ya maliasili.
Warsha hiyo iliwajengea uwezo maafisa wanaohusika na udhibiti wa biashara haramu bandarini kupitia vikosi vya Joint Ports Control Unit (JPCU), kwa kuwapa maarifa kuhusu mbinu zinazotumiwa na wahalifu kusafirisha maliasili kwa kutumia makontena.
Akizungumzia manufaa ya mafunzo hayo, mwakilishi wa TFS katika warsha hiyo, SCO Reuben Magandi, alisema ushirikiano wa kikanda utasaidia kuimarisha ulinzi wa maliasili zinazosafirishwa kwa kutumia makontena.
Magandi alisema washiriki walijifunza mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu katika mnyororo wa usafirishaji wa mizigo kwa makontena, maarifa ambayo yatasaidia kuimarisha udhibiti wa usafirishaji haramu wa maliasili.
Aidha, washiriki walipata mafunzo kuhusu utambuzi wa mimea inayolindwa chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea Iliyo Hatarini Kutoweka (CITES), pamoja na ukaguzi wa nyaraka za mizigo inayoingia nchini, inayosafirishwa nje ya nchi na inayopita nchini kuelekea maeneo mengine.
Warsha hiyo ilifadhiliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) na Umoja wa Ulaya (EU), kupitia vikosi vya udhibiti wa biashara haramu bandarini (JPCU), na ilishirikisha washiriki kutoka Benin, Ghana, Senegal, Togo, Kenya na Tanzania.
TFS inatarajiwa kunufaika na maarifa hayo katika kuimarisha juhudi za kulinda maliasili na kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka unaohusisha usafirishaji wa maliasili kwa kutumia makontena.