09
Nov
TANZANIA YAZIKARIBISHA NCHI SITA ZA AFRIKA KUSINI KWA MAFUNZO YA UZOEFU
Na.Naishooki Makeseni - MAELEZO.
Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kinara katika sekta ya ufugaji nyuki na kilimo misitu barani Afrika, baada ya kupokea washiriki kutoka nchi sita za Kusini mwa Afrika kwa ajili ya mafunzo ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora zinazotumika nchini katika usimamizi na uendelezaji wa sekta hizo.
Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika mkoani Tabora na yamewakutanisha washiriki kutoka nchi saba ambazo ni Tanzania, Zimbabwe, Angola, Zambia, Malawi, Namibia na Botswana katika jukwaa la kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu za kisasa za ufugaji nyuki na kilimo misitu.
Akifungua mkutano huo Jumatatu, Novemba 9, 2026, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Benard Patric Marselin, amesema Tanzania imepata heshima kubwa kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo kutokana na mafanikio yanayotambulika kimataifa katika usimamizi wa rasilimali za ardhi na misitu.
"Tuna bahati kubwa kupata wageni kutoka nchi mbalimbali ambao wamekuja kushiriki mkutano huu. Washiriki hawa kutoka Zimbabwe, Angola, Zambia, Malawi, Botswana na Tanzania wameamua kuja nchini kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka katika mafanikio yaliyopatikana," amesema Bw. Patric.
Ameeleza kuwa moja ya mambo muhimu yaliyoifanya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji ni fursa ya washiriki kujifunza kwa vitendo, ambapo pamoja na kupata mafunzo ya nadharia, watapata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali mkoani Tabora yanayotekeleza shughuli za ufugaji nyuki na kilimo misitu.
Amesema ziara hizo zitawawezesha washiriki kuona kwa karibu namna shughuli hizo zinavyofanyika, changamoto zinazojitokeza pamoja na mbinu zinazotumiwa kuongeza tija na uzalishaji.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali imeendelea kuweka juhudi katika kuimarisha sekta ya ufugaji nyuki na kilimo misitu hatua inayoifanya Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza barani Afrika katika usimamizi endelevu wa rasilimali za asili.
Akizungumzia fursa za kiuchumi katika sekta hiyo, Bw. Patric amesema Tanzania ina nafasi kubwa katika soko la asali barani Ulaya, huku akibainisha kuwa sehemu kubwa ya asali inayozalishwa kwa ajili ya soko hilo inatoka mkoani Tabora.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Misitu Tanzania, Dkt. Zainabu Bugwa, amesema ufugaji nyuki ni shughuli inayofanyika katika nchi nyingi duniani, ambapo kila nchi ina uzoefu na mbinu zake za uzalishaji.
Hata hivyo, amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee katika sekta hiyo kutokana na ukubwa wa shughuli za ufugaji nyuki na uwezo wake mkubwa wa kuzalisha asali.
Ameongeza kuwa kupokea washiriki kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kujifunza uzoefu wa Tanzania ni hatua muhimu inayodhihirisha kutambulika kwa mafanikio ya nchi katika sekta hiyo na kuongeza fursa ya Tanzania kuendelea kujitangaza kimataifa.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kukuza maarifa na kuhamasisha matumizi ya mbinu bora za ufugaji nyuki na kilimo misitu, huku yakiiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuendeleza uongozi wake katika sekta hizo barani Afrika.