25
Oct
SERIKALI YAZIDI KUBORESHA JESHI LA UHIFADHI: DKT. ABBAS AAGIZA MIRADI YA JESHI HILO KUKAMILIKA NDANI YA SIKU 90
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuliboresha Jeshi la Uhifadhi kwa kuliwezesha kifedha, kiutawala na kitaaluma, ili kulinda rasilimali za taifa kwa ufanisi na weledi mkubwa.
Akizungumza leo (Oktoba 25, 2025) katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Jeshi la Uhifadhi, Mlele mkoani Katavi, alipofunga rasmi mafunzo ya awali ya kijeshi kwa askari wapya 369 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na mafunzo ya uongozi kwa askari 311 wa TANAPA, Dk. Abbasi alisema serikali imejikita kuimarisha nidhamu, uzalendo na ufanisi wa watumishi wa sekta hiyo.
“Leo tumeshuhudia vijana wetu 369 wa TFS na wenzao 311 wa TANAPA wakihitimu mafunzo haya muhimu. Hili ni jambo la fahari kwa wizara yetu na taifa kwa ujumla,” alisema Dk. Abbasi.
Akimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa ajira mpya serikalini, Dk. Abbasi alisema wahitimu hao ni sehemu ya vijana walioajiriwa kufuatia kibali cha Rais kufungua fursa za ajira katika sekta ya maliasili na utalii.
“Rais wetu anatupenda. Hawa vijana 369 wa TFS na 311 wa TANAPA ni ushahidi wa uamuzi wake wa kuongeza nguvu kazi serikalini,” alisema huku akishangiliwa.
Alibainisha kuwa katika kipindi kifupi, Rais Samia ameidhinisha zaidi ya ajira 2,400 serikalini, ikiwemo zaidi ya 900 kwa taasisi za uhifadhi kama TFS, TANAPA, NCA na TAWA — hatua iliyoongeza uwezo wa usimamizi wa rasilimali asilia kwa nguvu kazi yenye maadili na weledi.
Aidha, Dk. Abbasi alitoa maelekezo ya siku 90 kwa taasisi za uhifadhi kuhakikisha changamoto zilizobainika katika Chuo cha Mafunzo ya Awali ya Kijeshi cha TFS Mlele zinatatuliwa. Alizitaka taasisi hizo kushirikiana kukamilisha ukarabati wa barabara ya Mlele–Maji Moto (km 60) na ile ya kuelekea Nyonga (km 30), TFS kutengeneza madirisha, milango, mbao na samani za chuo hicho, TAWA kujenga bwalo jipya la chakula, na NCA kujenga jiko la kisasa linalotumia nishati safi ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuishi kwa askari.
“Jeshi halishindwi. Ndani ya siku 90 nikirudi hapa nataka kuona barabara zinapitika, bwalo limekamilika na vifaa vipo. Tuache maneno, tufanye kazi,” aliagiza Dk. Abbasi.
Aliongeza kuwa endapo changamoto nyingine zitabaki, Wizara itahakikisha zinapatiwa ufumbuzi kupitia Mfuko wa Wanyamapori na Mfuko wa Misitu Tanzania (TAF).
Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alimshukuru Dk. Abbasi kwa kufunga mafunzo hayo, akisema uwepo wake umeongeza hamasa na kuonesha umoja wa vyombo vya uhifadhi.
“Ni faraja kuona vijana wetu wakihitimu chini ya uangalizi wa serikali. Wamejifunza nidhamu, uzalendo na weledi,” alisema Prof. Silayo.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo yalikuwa ya kipekee kwa kuwa yaliunganisha askari wapya wa TFS na maafisa wa TANAPA waliokuwa kwenye mafunzo ya uongozi, hatua iliyojenga mshikamano na uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya uhifadhi.
Prof. Silayo alimshukuru Rais Samia kwa kutoa vibali vya ajira zaidi ya 800 kwa TFS na ajira nyingine 300 zinazotarajiwa kutangazwa hivi karibuni, akisema, “Vijana hawa ni mashujaa wapya wa kulinda misitu na wanyamapori wa taifa letu.”
Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi Samuel Msuva alisema mafunzo hayo yaliyodumu kwa miezi minne yalihusisha masomo ya uzalendo, haki za binadamu, uongozi, matumizi ya silaha, uchunguzi wa jinai na ujanja wa porini, yakitolewa kwa ushirikiano wa JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Mahakama.
“Wahitimu wameonesha uwezo mkubwa wa kinidhamu na kimwili. Tupo imara kulinda rasilimali za taifa,” alisema Msuva.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Yahya Daudi Mbulu, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Alhaji Majid Mwanga, alisema Mlele imebarikiwa kuwa na misitu mikubwa ya hifadhi ikiwemo Rungwa River, Mlele Hills na Inyonga yenye zaidi ya hekari milioni 1.4, lakini inakabiliwa na uhaba wa watumishi kwani inahudumiwa na askari 14 pekee wa TFS.
“Tunaomba kwa heshima baadhi ya vijana 369 mliohitimu leo mupelekwe hapa Mlele. Kama wahenga walivyosema, charity begins at home,” alisema Mbulu.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wahitimu wapya kuzingatia kanuni za utumishi wa umma, akisisitiza nidhamu, bidii, uadilifu na utiifu kwa serikali, huku akiwakumbusha kufuatilia kwa umakini taarifa zao kwenye mifumo ya hifadhi ya jamii na kujaza kwa wakati mfumo wa PEPMIS unaotathmini utendaji kazi wa watumishi wa umma.