25
Aug
Rais Samia apongeza ushiriki wa TFS Kizimkazi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekabidhi cheti cha pongezi kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutokana na ushiriki wake wa kipekee katika Tamasha la Tisa la Kizimkazi lililofanyika Kusini Unguja, Zanzibar kuazia tarehe 18-25 Agosti, 2024.
Cheti hicho cha pongezi kilipokelewa kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof Dos Santos Silayo na Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia uzalishaji mbegu bora za miti Caroline Malundo pamoja na Meneja Mawasiliano, Johary Kachwamba katika hafla ya chakula cha usiku iliyofanyika Ikulu ndogo, Kizimkazi, Zanzibar.
Katika tamasha hilo, Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TFS lilivutia wadau wengi kwa kuanzisha zao jipya la utalii wa nyuki (Api-tourism), ambapo wageni walipata fursa ya kushuhudia na kushiriki katika shughuli zinazohusisha nyuki, ikiwemo uzoefu wa kudungwa na nyuki tofauti na ilivyokuwa katika matamasha ya miaka ya nyuma.
Zao hili jipya la utalii wa nyuki liliibua shauku na kuvutia watu mbalimbali waliotembelea TFS ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wadau waliohudhuria tamasha hilo walionyesha kupendezwa na ubunifu huu wa TFS, wakisifu juhudi za kuimarisha utalii wa kipekee na endelevu kupitia maliasili za nchi.
Sambamba na hayo kupitia zao hili la Utalii wa Nyuki wananchi walipata fursa ya kudungwa na nyuki, na kupewa elimu juu ya mazao ya nyuki yaliyoongezewa thamani kama vile asali, chavua, karanga za asali, maziwa ya nyuki ambavyo watu hutumia kama dawa na virutubisho katika mwili,’ anasema Kachwamba.