25
Sep

PANZI MWENYE RANGI YA BENDERA YA TAIFA KIVUTIO MAONESHO YA UTALII

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

DAR ES SALAAM. Panzi mwenye rangi zinazofanana na bendera ya Taifa amekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Maonesho ya Utalii yanayofanyika Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam.

Panzi huyo anayepatikana katika Msitu wa Hifadhi ya Asili Pugu-Kazimzumbwi, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, amevutia wageni baada ya kuonyeshwa picha yake na kupata maelezo kuhusu upekee wake kutoka kwa Mhifadhi wa Utalii wa hifadhi hiyo, Getrude Kimario.

Akizungumza katika maonesho hayo leo, Septemba 25, 2026, mmoja wa wageni, Joyce Milinga, alisema alivutiwa na taarifa za uwepo wa panzi huyo baada ya kuambiwa na rafiki yake ambaye ni raia wa nchi moja ya Asia.

“Kuna rafiki yangu mmoja aliniambia kuwa kuna panzi hawa Pugu ambao wanafanana na bendera ya Taifa. Taarifa hiyo ilinivutia na kuamua kufika hapa ili kujua zaidi,” alisema Milinga.

Kwa mujibu wa Kimario, panzi huyo hupatikana zaidi katika Msitu wa Hifadhi ya Asili Pugu-Kazimzumbwi kuanzia Novemba hadi Aprili, hali inayoufanya msimu huo kuwa fursa kwa wageni wanaotaka kuuona katika mazingira yake ya asili.

Alisema uwepo wa viumbe hao umeongeza mvuto wa utalii wa ikolojia katika hifadhi hiyo, huku TFS ikiendelea kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira yao pamoja na rasilimali nyingine za misitu.

“Msiishie kuona katika picha, karibuni muone mdudu huyu ambaye ni kivutio kwa wageni wengi wanaotembelea Hifadhi ya Pugu-Kazimzumbwi. Msimu wake ni kuanzia mwezi Novemba,” alisema Kimario.

Maonesho hayo yanafanyika kuelekea kilele cha Siku ya Utalii Duniani, kinachotarajiwa kufanyika Septemba 27, 2026, yakilenga pia kuhamasisha wananchi na wageni kutambua fursa mbalimbali za utalii wa ikolojia nchini.